Mkurugenzi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bw. Adam Fimbo akiongea na waandishi katika banda la taasisi hiyo kwenye maonesho ya biashara ya kimataifa TANTRADE barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam leo.
Bw. Sgifrid kutoka TMDA akitoa maelezo kwa mmoja wa wananchi waliotembelea katika banda hilo leo.
Meneja wa Mawasiliano na Elimu Kwa Umma Bi. Gaudensia Simwanza akijadiliana jambo na Afisa Mawasiliano Bw. Sigrid Mtei wakati maonesho hayo yakiendelea.
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),imesema kuwa inafanya utafiti wa Dawa za nguvu za kiume aina ya Viagra kwa kuangalia matumizi yake kwa ukubwa na yapo kwa kiasi gani ili waweze kutoa elimu sahihi kwa jamii.
Pia wameziwekea mkakati dawa aina ya P2 kwa lengo la kudhibiti uholela wa utumiaji wake ambapo imeonekana watoto wa shule wengi wanapenda kuzitumia kutolea mimba.
Akizungumza hayo mapema leo jijini Dar es Salaam katika Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba ambayo msimu huu ni ya 46, Mkurugenzi wa TMDA, Adam Fimbo wakati akiongea na waandishi alisema ni muhimu kabla ya mtu kutumia dawa kufuata ushauri wa daktari.
Alisema utumiaji holela wa dawa za jamii ya kutolewa mimba na za kuongeza nguvu za kiume zimekuwa zikitumika ndiyo sivyo na kuwaleta madhara watu.
“Tumekuwa tukipata ripoti mbalimbali,watu wamekuwa wanapoteza maisha… wito wetu mkubwa mtu akitaka kutumia hizi dawa ni vema apate ushauri kwa mtaalamu wa afya,”alisema na kuongeza
“Kuna matukio mengi ya watu kupoteza maisha na wengine kupata shinikizo la damu kuzidi kuongezeka kwa kasi,”alisema.
Aidha alisema kazi yao kubwa ni kuelimisha umma juu ya matumizi ya dawa kwani hazipaswi kutumiwa kiholela kutokana na madhara yake kwa mwili wa binadamu.
Fimbo alisema kwa upande wa dawa za P2 nazo zimekua zikitumiwa na watoto wa shule kwaajili ya kutoa mimba.
“Tumeweka mkakati wa kuhakikisha tunatoa elimu kwa watoto wetu wa kike na wanawake kuacha kutumia dawa hizi kiholela kwa sababu zinasababisha vifo visivyotarajiwa na kuelimisha jamii matumizi sahihi ya kutumia,” alisema.
Wakati huo huo akiongelea udhibiti wa Dawa Bandia, Fimbo alisema wameweka mfumo wa ukaguzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo bandarini hadi katika masoko na kazi ya ukaguzi ufanyika kila siku.
Alisema dawa bandia ni dawa zilizotengenezwa kwa makusudi ya kudanganya au kuficha uhalisia wakebkwa njia ya vifungashio,lebo au viambata vinavyotumika.
“Kazi yetu kubwa ni kuzikamata na matukio kama haya yapo na endapo tukibaini tunawakamata tunafanya ukaguzi na kushirikisha Jeshi la Polisi,” alisema.