NA
KHALFAN SAID, SABASABA
KATIKA
kuhakikisha Wastaafu wanapata huduma kwa haraka na kwa urahisi zaidi, Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeanzisha mfumo wa
kielektroniki wa kuhakiki taarifa kwa kutumia alama za vidole (biometric),
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko huo Bw. James Mlowe amesema.
Bw.
Mlowe ameyasema hayo leo Julai 2, 2022 wakati akiwahamasisha Wastaafu na Wanachama
wa Mfuko huo wakiwemo wananchi kutembelea banda namba 13 la Ushirikiano baina
ya PSSSF na NSSF kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es
Salaam katika viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba barabara ya Kilwa
jijini.
“PSSSF
tuna wastaafu wanaopokea pensheni kila mwezi zaidi ya 160,000, ni utaratibu wa
kisheria na kikanuni kwamba Mstaafu anatakiwa kujihakiki mara moja kila mwaka”
alisema
Alisema
lengo la kuhakiki ni kutaka kujua kuwa taarifa za wastaafu wanaopokea pensheni kila mwezi zimebadilika au ziko vile vile,
zoezi hili limekuwa likifanyika kwa miaka mingi ingawa limekuwa na changamoto
mbalimbali.
“Badala
ya utaratibu wa awali wa Mstaafu kufika ofisini na kujaza fomu na kuja na
viambatanisho mbalimbali tumeona mfumo huu unaleta usumbufu kwahivyo tumekuja
na suluhisho ambapo Mstaafu anaweza kujihakiki kwa kutumia alama za vidole (biometric)
ambapo mwanachama anaweza kujihakiki sehemu yoyote.” Alifafanua.
Aidha
Meneja huyo alisema kwenye siku za usoni mwanachama anaweza kutumia simu janja
na kujihakiki popote na wakati wowote.
Amewahimiza
wastaafu na wanachama wa PSSSF wanaotembelea Maonesho hayo kufika kwenye banda
namba 13 ili waweze kujihakiki na kuchukuliwa alama zao za vidole na kwa hali
hiyo huduma ziweze kuwafikia huko waliko.
“Miundombinu
yote inayopatikana kwenye ofisi zetu zilizoenea nchi nzima inapatikana hapa sabasaba
kwa hivyo mwanachama, mwanachi, fika kwenye banda letu la ushirikiano na NSSF
ili tuweze kukuhudumia na kukupa elimu ya hifadhi ya jamii.” Alisema.
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, PSSSF, Bw. James Mlowe (kulia) akiwahudumia wanachama kwenye banda la Mfuko huo viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam Julai 2, 2022.
Mwanachama akihudumiwa
Mwanachama akihudumiwa
Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, PSSSF, Bw. James Mlowe (kulia) akizungumza na Afisa Uhusiano Mwandamizi, NSSF, Bw. Sebera Fulgence kwenye banda la Ushirikiano namba 13 linalotumiwa kwa pamoja na Mifuko hiyo ya Hifadhi ya Jamii.
Mwnaachama akipitia taarifa zake za Michango, baada ya kuhudumiwa.