……………..
Na Joseph Lyimo, Mbulu
Ili kuhakikisha Mkoa wa Manyara, unapiga hatua kubwa kwa wananchi wake kushiriki chanjo ya UVIKO-19 na kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo, viongozi wake wamejipanga kuhakikisha wanatembea nyumba kwa nyumba kwa ajili ya kufanikisha hilo.
Manyara, wameanza kampeni maalum ya kuwachanja wananchi wa mkoa huo dhidi ya UVIKO-19 kwa kutembea nyumba kwa nyumba ili kuwafikia watu wa jamii zote na walio katika mazingira magumu.
Kutokana na hali hiyo, jamii ya wafugaji, wakulima, wavuvi, wachimba madini, wafanyabiashara, watumishi wa umma, taasisi, asasi na wananchi wa Mkoa wa Manyara kwa ujumla wanaostahili kupata chanjo ya UVIKO-19 watanufaika na huduma hiyo.
Katika zoezi la kuchanja wananchi dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huo wa UVIKO-19, ambapo Mkoa wa Manyara unatajwa kushika nafasi ya mwisho kitaifa kwa kuchanja wananchi wake, viongozi na wadau wamejipanga kuhakikisha hivi sasa wanapiga hatua.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Karolina Mthapula anasema kwamba wamejipanga kuhakikisha kuwa wanafikia malengo waliyojiwekea ili wananchi wote wanaostahili kupata chanjo ya UVIKO-19 wanachanjwa.
“Wataalam wa afya ambao watakuwa wanatoa chanjo ya UVIKO-19 kwenye mkoa wa Manyara na watakuwa wanatembea nyumba kwa nyumba kuhakikisha wanatoa chanjo kwa watu wote wanaostahili baada ya kupata elimu juu ya chanjo hiyo,” anaeleza RAS Mthapula.
Hata hivyo, RAS Mthapula amewataka watendaji wa mkoa huo na wa wilaya tano za Manyara kuhakikisha kuwa kuhamasisha wananchi ili wajitokeza na kupata chanjo dhidi ya UVIKO-19.
Hadi sasa mkoa wa Manyara umetoa chanjo kwa watu 300,000, idadi ambayo ni sawa na asilimia 3.7 tu ya lengo ya lengo la wananchi 956,000 walilojiwekea.
Akizungumza mjini Babati wakati wa kikao kazi cha tathmini ya utoaji chanjo ya UVIKO -19, Meneja wa mpango wa chanjo wa Taifa wa Wizara ya Afya Dkt Florian Tinuga anasema hadi sasa mkoa wa Ruvuma ndiyo unaoongoza kitaifa kwa kufikia asilimia 40 ya uchanjaji.
Dkt Tinuga anaeleza kwamba lengo la kitaifa ni kuhakikisha kuwa wanafikia lengo la kufikia asilimia 70 ya kutoa chanjo dhidi ya UVIKO -19 ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
Mkazi wa kijiji cha Qatesh wilayani Mbulu, Johnston Haimu anasema kuwa mpango wa wataalam wa mkoa wa Manyara kupita nyumba hadi nyumba, utasaidia wananchi wake wengi kupata chanjo ya UVIKO-19.
“Japokuwa hamasa haikuwa kubwa kwa kipindi kilichopita kwa watu kupata chanjo pia watu wengi hawakupoteza maisha kama tulivyosikia mikoa mbalimbali ikiwemo Kilimanjaro,” amesema Haimu.
Anasema watu wengi hawakushiriki kuchanja chanjo ya UVIKO-19 kutokana na watu wachache mkoani Manyara, kupoteza maisha kwani endapo vifo vingetokea mfululizo wangechanja wengi.
“Mimi binafsi nilipatiwa chanjo ya UVIKO-19 ila nawaasa wananchi wenzangu ambao hadi hivi sasa hawajapata chanjo washiriki kuchanjwa kwani ukiupata huo ugonjwa ukiwa haujachanjwa unapata madhara makubwa,” anasema Haimu.
Mkazi wa kata ya Sanu wilayani Mbulu, Christopher Zebedayo amepongeza mpango wa serikali mkoani Manyara, wa kupita nyumba hadi nyumba ili wananchi wake wapate chanjo ya UVKIO-19.
“Wengi wao watakuwa na hamu ya kupata chanjo baada ya kusikia kuwa wataalam watapita nyumba hadi nyumba ili kutoa chanjo ya UVIKO-19 kwa wananchi mbalimbali,” anamalizia kwa kusema Zebedayo.