Mchumi Mwandamizi na Kaimu Meneja wa sehemu ya ununuzi wa Mbolea kwa pamoja -TFRA Elizabeth Bolle akielezea kuhusu ushiriki wa Mamlaka hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya biashara Sabasaba ambayo yameanza leo mpaka July 13 Mwaka huu.
Kaimu Meneja Uzalishaji wa Ndani na Mazingira TFRA Stephen Ngoda akielezea kuhusu ushiriki Mamlaka hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya biashara Sabasaba ambayo yameanza leo mpaka July 13 Mwaka huu na namna watakavyowahamasisha wawekezaji kutoka nje ili kuweza kuongeza uzalishaji Mbolea.(picha na Mussa Khalid)
…………………
NA MUSSA KHALID
Mamlaka ya udhibiti wa Mbolea nchini -TFRA imewahamasisha wawekezaji wa ndani kupanua wigo wa viwanda vyao vya Mbolea Ili kupata soko la ndani na kupunguza utegemezi wa mbolea zinazotoka nje ya nchi.
Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na Mchumi Mwandamizi na Kaimu Meneja wa sehemu ya ununuzi wa Mbolea kwa pamoja -TFRA Elizabeth Bolle wakati akifanya mahojiano na mwandishi wa habari hizi kuhusu ushiriki wa Mamlaka hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya biashara Sabasaba ambayo yameanza leo mpaka July 13 Mwaka huu yenye kauli mbiu isemayo Tanzania ni mahali sahihi pa biashara na uwekezaji.
Bolle amesema kuwa lengo la Mamlaka hiyo ni kudhibiti ubora na Biashara ya Mbolea kwenye Mnyoro wa thamani kuanzia kwenye uzalishaji, uingizaji wa Mbolea kutoka Nje,kuhifadhi usambazaji na uuzaji wa Mbolea ndani na Nje ya Nchi.
Aidha amesema Mwaka huu TFRA inashiriki kwa mara ya pili katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba kwa lengo la kujitangazai ili kufahamika kwa jamii lakini pia kutoa elimu ya kufata taratibu kwa wadau wa Mbolea Nchini sambamba na kuhamasisha Uwekezaji wa Mbolea Nchini.
“Tunatarajia baada ya maonyesho jamii na wadau mbalimbali watakuwa na uelewa Juu ya uwepo wa Mamlaka na huduma zinazotolewa pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na Muamko Mkubwa wa wawekezaji kutoka ndani na Nje amabao watakakuja kuwekeza Nchini.”amesema Bole
Amesema mpaka sasa kuna miradi mitatu inaendelea ukiwemo wa uwekezaji wa Kampuni ya Intracom kutoka nchini Burundi ambayo imewekeza kiwanda cha kuzalisha Mbolea ambacho kinatarajiwa kuzalisha kiasi cha Tani laki sita za mbolea kwa mwaka na tani laki tatu za visaidizi za mbolea.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Uzalishaji wa Ndani na Mazingira TFRA Stephen Ngoda amesema wataendelea kuwahamasisha wawekezaji kutoka nje ili kuweza kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa mbolea zinazotoka nje ya nchi.
Ngoda amesema mpango mkakati wa taasisi hiyo ni kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuhakiksha ifikapo mwaka 2025 wapunguze utegemezi kwa asilimia 25.
‘Nchi yetu inarasilimali nyingi ambazo zinaweza kutengenezea mbolea hivyo ni jukumu letu kuwaeleza wawekezaji na kuwaelezesha kwamba tuna uhitaji huo na pia kuwaeleza kuwa soko la mbolea ambalo lipo nchini linauhitaji wa kiasi gani nchi zinazotuzunguka pia hivyo wakati huu wa sabasaba tutajitahidi kuwaelewesha’amesema Ngoda
Hata hivyo wito umetolewa kwa wawekezaji wa ndani na Nje ya Nchi kutambua kuwa tasnia ya mbolea ina fursa kubwa ya uwekezaji kwani Watanzania wanatumia Takriban tani laki nne mpaka tano za mbolea lakini asilimia 90 zinaagizwa kutoka nje.