Adeladius Makwega-BUJORA MWANZA
Katkati ya 2008 nikiwa nakaribia kuhitimu Shahada ya Sanaa ya Habari ya Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa kwa kuwa nilikuwa miongoni mwa viongozi katika serikali ya wanachuo tuliaaza kukabidhi madaraka kwa wenzetu waliokuwa mwaka wa pili, sambamba na uongozi wa CCM wa tawi kwa maana nilikuwa katibu wa CCM tawi wa Itikadi na Uenezi.
Kabla ya kuhitimu nilipozungumza na mzazi wangu kuhusu kuendelea na Shahada ya Uzamili baada ya kuhitimu alikubaliana nami niendelee nayeye kunilipia karo tu ya masomo hayo ya miaka miwli lakini mimi binafsi nijilipie huduma nyengine ili niweze kusoma kozi hiyo.
Karo ya masomo hayo kwa mwaka mmoja ilikaribia milioni 2.7, huku mshahara wangu ulikuwa ni shilingi 108,080/- kwa mwezi.
Uongozi wa wanafunzi tulikabidhi vizuri sana Rais wa Serikali ya Wanachuo alikuwa Mheshimiwa Antipas Zeno Mngungusi Mbunge wa Malinyi mkoani Morogoro kwa sasa, mimi nikiwa makamu wake.
Makabidhiano yalihamia katika tawi la CCM la chuo hiki. Kwa kuwa nilikuwa nimenuia kuendelea na masomo ya shahada ya uzamili niliamua kuchukua fomu ya Uenyekiti wa tawi la CCM kugombea.
Viongozi wa tawi hili waliokuwa wanamaliza muda wao alikuwepo Silanda Mgombela(Sasa ni Profesa) na Yotham Ndembeka,(Mkiti) Dikcson Mnumbi(Katibu Tawi) Kazimbaya Makwega (Katibu Muenezi), Minge Mhondo (Katibu Uchumi na Fedha), . Yatera Yateri(Mkiti Vijana). Mheshimiwa Ngolo Malenya(Katibu UWT)–Sasa Mkuu wa wilaya ya Ulanga
Fomu za kugombea zilichukuliwa na kurejeshwa na majina ya wagombea kwa nafasi zote yalitajwa na siku ya uchaguzi ikafika, msimamizi wa uchaguzi huo alikuwa Katibu wa UVCCM mkoa wa Iringa wakati huo Ndugu Ndolangu.
Wakati huo Katibu wa CCM mkoa wa Iringa alikuwa ni Ndugu Kilumbi Ngenda sasa ni Mbunge wa Ujiji Kigoma. Mheshimiwa Ngolo Malenya wakati huo akiwa mwaka wa pili akiingia mwaka wa tatu shahada ya kwanza ya sheria yeye alishinda uenyekiti wa vijana wa tawi kwa kura nyingi sana.
Zamu ya kujinadi kwangu ilifika, kwanza alitangulia mgombea mwezangu ninayekumbuka jina lake moja tu la Mahona, alipomaliza ikafika zamu yangu.Nikajinadi na kuomba kura, mwanakwetu ukafika wakati wa maswali.
Wanachama wenye tawi lao waliibuka na mikono juu ya maswali mengi. Ndugu mgombea wewe unahitimu chuo Novemba 2008 iweje leo hii unagombea uongozi wa tawi letu la CCM?
Nilijibu swali hilo nikisema kuwa jamani binafsi ninakusudia kurudi hapa chuoni mwezi wa tisa kama mwanafunzi wa shahada ya uzamili, hilo msiwe na shaka nalo kabisa. Nikapigwa na swali lingine je wewe unauhakika gani kama utafaulu mitihani yako ya mwisho? Nikajitetea mno. Mikono ya maswali ikawa mingi dhidi ya mgombea.
Msimamizi wa uchaguzi huo kwa kuwa alikuwa ni mwanasiasa mzuri sana , anayejiamini mno akasimama akaomba utulivu kwanza ukumbini, alafu akasema kidumu Chama cha Mapinduzi wanachama wakajibu kidumu.
“Jina la mgombea aliye mbele yenu, chama kimelirudisha si kwa upendeleo wowote ule ana vigezo na sifa kama walivyo wagombea wengine, tambueni kitu kimoja, matawi ya CCM ya vyuo vikuu yanawajumuisha wanafunzi, walimu, wafanyakazi wa vyuo hivi na hata mtu aliye jirani na eneo hili, awe anasoma au la. Jina hilo na majina ya wagombea wengine yapo mbele yenu kwa maamuzi ya kura, waamuaji ni nyinyi. ”
Akauliza kuna swali lingine ? Kimya, Haya gaweni karatasi za kupiga kura, alisema.
Kura zilipigwa, matokeo yaliyotangazwa na mimi kupata kura saba, huku ndugu Mahona kapata kura 93, Ndugu Mahona alishinda kwa kishindo na kuwa mwenyekiti.
Hayo ndiyo yalikuwa maamuzi ya wenye chama chao, nilikumbuka namna tulivyokuwa tunasimamia ujenzi wa tawi mimi na Dickson Mnubi miaka ya nyuma lakini wanachama hawakuliona, hilo wakati wao wapo likizo nyumbani kwao. Hapo hata ukinuna shauri lako maamuzi yameshafanywa na wanachama.
Mwezi wa tisa 2008 ulipofika nilianza shahada yangu ya uzamili vizuri kabisa huku kukiwa na vikao vya tawi vya chama chetu ninashiriki kama mwanachama na huku wakinitambulisha kama katibu muenezi mstaafu. Katika viongozi wa tawi hilo ninawakumbuka Mwenyekiti aliyenishinda ndugu Mahona na Katibu tawi Nashoni Kayoka, mwenyekiti wa vijana Mheshimwa Ngolo Malenya.
Hawa ndugu kila walipokuwa na jambo gumu walinitafuta tunashauriana, likiwa gumu sana tunamfuata Katibu wa CCM mkoa wa Iringa ndugu Ngenda anatusaidia mawazo, tunarudi shuleni kusoma.
Shauri moja ambalo ninalikumbuka, usiku mmoja nilipigiwa simu na viongozi hawa, nikafika walipo tukazungumza jambo la uchaguzi wa serikali ya wanachuo ambapo wagombea waliokuwa wanahisiwa kuwa hatari ni Seleimani Serera na Godwini Kunambi sasa ni Mbunge wa Mlimba) na chaguo la chama lilikuwa ni Amani Nduhije.
Amani Nduhije alikuwa mwanaccm tangu anafika chuoni mwaka wa kwanza, Seleimani Serera pia hivyo hivyo, shida ilikuwa ni kwa Godwin Kunambi na misimamo yake mikali, Je ni mwanaccm? Ilikuwa kazi sana kupata majibu ya taarifa za Kunambi, lakini baadaye watu watatu waliukata mzizi wa fitna.
Chuoni hapo kulikuwa na vijana wawili Kulwa na Doto wake ambao walikuwa Chipukizi wa CCM tangu wakiwa wadogo, wao walisema wanamfahamu Kunambi ni kijana mzuri.
Abdul Zulu Liyana yeye akitokea eneo moja na Kunambi nilipowasiliana naye alituhakikishia kuwa Kunambi ni mwanaccm, tusihofu juu ya siasa zake hata kama anaonekana ana siasa kali lakini chama anakiheshimu mno. Kwa bahati mbaya majina ya Kunambi na Serera hayakurudisha na kamati ya uchaguzi ya Chuo kupigiwa kura jina lililorudi ni jina la Amani Nduhije na hata kura zilipopigwa alishinda ndugu huyu na kuwa na Rais wa wanachuo.
Hapo mwanakwetu mimi bado ninasoma, sasa akina Mahona muda wao ulikwisha na kukafanyika uchaguzi wa viongozi, mimi nikagombea uenyekiti nikashinda kwa kura nyingi mno na Katibu Muenezi aliyeshinda alikuwa Mheshimiwa Seleiman Serera.
Baadaye Godwini Kunambi akachaguliwa kuwa katibu wa serikali ya wanachuo huku akiwa kiongozi mzuri sana.
Nilikuja kumfahamu kuwa mheshimiwa Godwin Kunambi anatoka katika ukoo wa Chifu Kunambi, nikabaini kuwa ukoo wa Chifu Kunambi.-Hii ndiyo familia iliyokuwa inamiliki eneo ambalo leo hii ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na eneo hilo familia hiyo ililitoa bure kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu hiki. Mwanakwetu upo?
Mwanakwetu unaweza kujinasibu kuwa wewe umesoma chuo kikuu cha Dar es Salaam au ukajinasibu kuwa wewe ni Daktari wa Falsafa uliowahi kufundisha chuo kikuu hiki. Mwanakwetu tambua kuwa wenzako eneo hilo lilikuwa mali yao wakizikia hadi ndugu zao na wakalitoa bure ili Watanzania wengine wasome. Je wewe umetoa nini?
Wapo akina Kunambi wengi wanaokosa nafasi za kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Lakini hawalalamiki, mwanakweru na bado akina Kunambi wengi wataendelea kukosa nafasi zakusoma chuo hiki na hata hao wanaochagua hawatambua hili jambo lililofanywa na ukoo huu kwa kuwa sasa vigezo ni kufaulu tu na si nasaba.
Kwa nini leo ninayasema haya? Suala la Kunambi na Waziri Ardhi lilinisikitisha mno, Mungu bahati spika wa Bunge letu Mheshimiwa Tulia Ackson ameshalimaliza, mgogoro huo ulinikumbusha tukio la miaka inayokaribia 14 maisha yetu ya Chuo Kikuu.
Kwako Mheshimiwa Kunambi haupaswi kurudi nyuma, endelea kusonga mbele kwa kuwatetea wanyonge, kile kitendo kilichofanywa na Chifu Kunambi ni sadaka kubwa kwa Tanzania yetu ambayo wengine ndiyo wanaisoma katika matini hii kwa mara ya kwanza.
Mwanakwetu itoshe kuishia hapa kwa leo.
makwadeladius @gmail.com
0717649257