Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kuanza mchakato wa kumhamishia kwenye shule iliyoko Tunduru mjini Mwalimu Judith Sichalwe mwenye miaka 29 (mwanamke anayeonekana kwenye picha) ambaye amejifungua watoto wanne bila upasuaji katika hospitali ya Wamisionari ya Mbesa iliyoko Tunduru.
DC Mtatiro ametoa maelekezo hayo alipomtembelea Mwalimu huyo katika kijiji cha Mkapunda katika Shule ya Msingi Mkapunda iliyoko kilomita 100 kutoka Tunduru Mjini ambako anafundisha.
Mtatiro ameeleza ni wajibu wa serikali ya wilaya ya Tunduru kumrahisishia maisha mwalimu huyo ambaye anaweza kukabiliwa na hatari ya kushindwa kumudu gharama za maisha kutokana na idadi hiyo ya watoto wachanga kwa wakati mmoja.
Afisa Tarafa wa tarafa ya Nalasi ambako mwalimu Judith anaishi, Salumu Kijumu, ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kuratibu misaada mbalimbali, lakini pia amewaomba watanzania wote watakaoguswa na kazi ya malezi ya pacha hawa wanne kumsaidia mwalimu huyo.
DC Mtatiro ameelekeza kuwa mtanzania atakayeguswa na akahitaji kumsaidia Mwalimu Judith Sichwale asisite kuwasiliana na Mwalimu Judith moja kwa moja kupitia namba ya Tigo 0673 103 536 iliyosajiliwa kwa majina Judith Sichwale.