Kilimanjaro; Kijana wa Miaka 13, Brian Hurt ameibuka mshindi wa kwanza katika mashindano ya pikipiki ya West Kili Forest Tour Challenge yaliyofanyika katika msitu wa asili uliopo kwenye Shamba la Miti West Kilimanjaro wilayani Sia mkoani Kilimanjaro.
Mashindano hayo yalihusisha nchi mbalimbali zikiwa na wachezaji 7, huku bara la Afrika likiwakilishwa na Tanzania na Kenya yalifanyika jana Julai 25, 2022 ambapo Brian Hurt aliyekuwa akitumkia pikipiki aina ya Honda 125cc aliweza kujinyakulia ushindi huo.
Akizungumza mara baada ya kuibuka mshindi kijana huyo raia wa Uingereza aishiye nchini anasema amekuwa akiendesha pikipiki na baba yake tangu akiwa na umri wa miaka nane na amefurahi kuibuka mshindi huku baba yake akiibuka mshindi wa nne.
Wambui Muriithi raia wa Kenya alifanikiwa kuibuka mshindi wa pili huku akifuatiwa na mshirika wake toka chama cha Waendesha Pikipiki wanawake Kenya, Abbie Ndanyi aliyeshika nafasi ya tatu
Muriithi anasema wao hupenda kuendesha pikipiki kujifurahisha na kujivinjari na kupitia mashindano hayo ‘wameinjoi’ na kutoa wito kwa waendesha pikipiki wengine duniani wanaopenda ‘adventure’ kujitokeza kwa wingi mwakani.
Awali akifungua mashindano hayo Mkuu wa Wilaya ya Siha Thomas Apson katika uwanja wa Simba Farm Lodge alisema katika kuunga mkono juhudi za mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kutangza utalii wameona wafanye mashindano ya pikipiki, baiskeli, marathon na watembeaji ndani ya hifadhi.
“Mwaka jana wakati naamia wilaya hii niliitwa kufungua mashindano haya, na tangu hapo nikasema tuendelee kuyafanya kwani michezo ni afya lakini pia ni sehemu ya utalii ukizingatia washiriki watapita sehemu za wanyamapori lakini pia msituni,
“Niwashukuru TFS na wadau wengine kwa kudhamini mashindano haya, mwaka jana yalifanyika katika hali ngumu lakini niombe wadau wengine wasisite kutushika mkono mwakani,” alisema.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba la West Kilimanjaro Masawanga Ismail amesema “gari limewaka, tamasha hili litakwenda kufanyika tena mwakani kutoa fursa ya watu kwenda kuona mapango, bwawa, wanyama na misitu iliyohifadhiwa.
Naye Mratibu wa tamasha hilo Mensiur Elly alisema tamasha hilo ni la siku mbili ambapo siku ya kwanza imekwisha kwa kuhusisha mashindano ya pikipiki na baiskeli (washiriki 31 walijitokeza) huku siku ya pili ikihusisha marathon na watembea kwa miguu.
Washiriki wote wa shindano hilo walipewa medali huku washindi wa tatu (wakwanza, wapili na tatu) wa Baiskeli wakipewa medali, fulana pamoja na bahasha zilizokuwa na fedha.
Mashindano ya West Kili Forest Tour Challenge yamedhaminiwa na Kampuni mbalimbali ikiwemo TFS ambayo ilitoa fedha taslimu pamoja na sehemu ya eneo lake kutumika, World Vision, Leadership School, Simba Farm lodge, Notice Kilimanjaro, AU YAFTEMOPA, Halmashauri ya Wilaya ya Siha na Bonite