Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Dkt. Naomi Katunzi akiwahutubia Wanafunzi 823 waliohitimu katika Taasisi hiyo wakati wa Mahafali ya 58 yaliyofanyika Juni 24, 2022 jijini Dar es Salaam. .
Wanafunzi waliohitimu ngazi mbalimbali za elimu ikiwemo Shahada wakifurahia mahafali yao yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Juni 24, 2022.(Picha na Mpiga Picha Wetu)
……………….
Wanafunzi 823 Wahitimu TEWWNa Mwandishi wetu- TEWWWanafunzi 823 wamehitimu masomo yao katika Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) katika kipindi cha mwaka wa masomo 2021/2022.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi hiyo Dkt. Naomi Katunzi wakati wa mahafali ya 58 yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Juni 24, 2022.
“ Jumla ya wahitimu 848 (Wanaume 298 sawa na 35 %, Wanjawake 550 sawa na 65 %,) wa elimu ya watu wazima wameweza kufuzu masomo kupitia programu mbalimbali zinazoendeshwa na TEWW, zikiwemo Elimu ya Watu Wazima na Mafunzo Endelezi (Adult and Continuing Education), Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii (Adult Education and Community Development) pamoja na Elimu Masafa (Distance Education).” Alisisitiza Dkt. Katunzi
Akifafanua Dkt. Katunzi amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa mpango wa kuwarejesha shuleni wasichana walioshindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito hali iliyowawezesha wengi wao kunufaika na elimu kupitia TEWW.
Aidha, Dkt. Katunzi ameitaka TEWW kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kusaidia kukuza Taasisi hiyo. Pia aliwataka wahitimu hao kwenda kufanya kazi kwa bidii na kuepuka vitendo vya uzembe.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TEWW Dkt. Michael Ngumbi amesema kuwa kati ya wahitimu hao, mhitimu 1 (me) ni ngazi ya shahada, wahitimu 823 (me 289, ke 534) ngazi ya stashahada na wahitimu 24 (me 8, ke 16) ni ngazi ya astashahada. mkoa wa Iringa wenye wahitimu wengi zaidi siku ya leo Mkoa huo una jumla ya wahitimu 161, ambayo ni asilimia 20 ya wahitimu ya wahitimu wote.
Mikoa mingine yenye wahitimu wengi ni Songwe (78), Dar es Salaam (77), Dodoma (52) na Kagera (50).Alieleza kuwa TEWW imeboresha mitaala ya stashahada na shahada ili wanachuo wapate semista nzima ya kujifunza kwa vitendo kwa kuanzisha na kuendeleza vituo vya kisomo.
Wanachuo wameweza kuanzisha vituo nchi nzima vyenye jumla ya wanakisomo wanaokaribia elfu sita. Mpango wa TEWW ni kuwa na vituo vyenye wanakisomo wapatao elfu kumi kila mwaka, ambavyo vinawezeshwa na wanachuo wakati wa semista ya mafunzo kwa vitendo.
Uwepo wa programu hizi za shahada, stashahada na astashahada, umewezesha taasisi yetu kuwaandaa walimu na wasimamizi wa EWW ambao wanao ujuzi na utayari wa kwenda kuanzisha na/au kuendeleza kisomo na EWW katika maeneo yao ya kazi.