Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wapili kushoto) alipowasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mlele. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Philbert Sanga.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akizungumza wakati wa ziara yake Wilayani Mlele. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Philbert Sanga na kulia ni Meneja RUWASA Mkoa wa Katavi, Mhandisi Peter Ngunula.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kushoto) akimsikiliza Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mlele, Mhandisi Gilbert Isack (kushoto) wakati wa ziara yake kwenye mradi wa ujenzi wa Bwawa la Maji la Nsekwa.
Muonekano wa Bwawa la Maji la Nsekwa Wilayani Mlele
……………………
Na Mohamed Saif
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amemuelekeza Mkandarasi anayejenga mradi wa Bwawa la maji la Nsekwa Wilayani Mlele kampuni ya Hematec Investment Ltd ya Dar es Salaam awe amekamilisha ujenzi wake ifikapo Mwezi Desemba mwaka huu.
Mhandisi Sanga ametoa maelekezo hayo Wilayani Mlele Mkoani Katavi Juni 23, 2022 alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa bwawa hilo linalotarajiwa kunufaisha wakazi wapatao 68,426 wa vijiji 16 kutoka Kata za Inyonga, Utende, Nsekwa, Ilela na Kamsisi.
Awali akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Mhe. Philbert Sanga alimuelezea Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Sanga kuhusu kusuasua kwa ujenzi wa bwawa pasi na sababu za msingi.
“Ninawapongeza sana Wizara ya Maji, kazi mnayofanya ni kubwa na sote ni mashahidi tunakiona mnachokitekeleza. Kabla ya ziara yako alitutembelea Mheshimiwa Waziri na alituahidi kwamba utakuja kufuatilia ujenzi wa miradi wilayani hapa na hili limetimia, hii inadhihirisha uchapakazi wenu,” alisema Mhe. Mkuu wa Wilaya.
Akiwa katika eneo la mradi ili kushuhudia kinachoendelea, Mhandisi Sanga hakuridhishwa na hali ya utekelezwaji wake hasa ikizingatiwa kuwa mradi huo umechukua muda mrefu kukamilika licha ya Mkandarasi kulipwa fedha zake kwa wakati
“Kazi hairidhishi, nilitarajia kukuta Mkandarasi anaendelea na kazi lakini bahati mbaya sana hakuna kinachoendelea, tumeleta fedha za kutosha hapa sijaridhika na ninachokishuhudia,” alisema Mhandisi Sanga.
Alisema Wizara ilikwamua miradi mingi ambayo ilikua ikisuasua maarufu kama miradi chechefu na hayupo tayari kushuhudia hali hiyo ikijirudia na kwamba anachohitaji ni kuona kazi ikiendelea kwa kasi ili kuwaondolea adha wananchi.
Katibu Mkuu Sanga alisisitiza kuwa Wizara ya Maji imekwishajipambanua mapema kuwa haitoendekeza wakandarasi wababaishaji kama ambavyo Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyoelekeza.
“Mhesimiwa Rais Samia alikwishatupatia maelekezo na mara nyingi Waziri wangu amekuwa akiyarejea maelekezo haya kwa wataalam wetu na wakandarasi kila anapotembelea miradi; tunachokifanya sisi ni utekelezaji. Hatuwezi kurudi huko tulikotoka, kama suala ni fedha semeni, hatupo tayari kudanganywa kwa uzembe wa mkandarasi,” alisisitiza Mhandisi Sanga
Mhandisi Sanga alisema baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakijificha kwenye kisingizio cha fedha jambo ambalo alisema halina ukweli wowote kwani kwa utaratibu wa sasa wa Serikali kupitia Wizara ya Maji malipo yanatoka kwa wakati pindi Mkandarasi anapowasilisha hati ya madai.
Alimuelekeza mkandarasi kuhakikisha bwawa hilo linakamilika ifikapo Mwezi Desemba mwaka huu ili msimu wa mvua unapochanganya ukute tayari bwawa limekamilika na alisisitiza kuwa ikitokea mkandarasi akachelewesha basi akatwe malipo yake.
“Maelekezo ya Wizara kwa Mkandarasi ni kuhakikisha mradi unakamilika kabla ya Mwezi Desemba mwaka huu, mvua zinapoanza bwawa linakuwa liko tayari,” alielekeza Mhandisi Sanga.
Naye mkandarasi kupitia mwakilishi wake, Elimring Molth alimuahidi Mhandisi Sanga kuwa bwawa hilo litakamilika kama alivyoelekeza na kwamba ifikapo Jumamosi ya tarehe 25 mwezi huu, timu ya wataalam wake itakuwa imewasili eneo la mradi na kuendelea na kazi.
Mhandisi Sanga aliiomba Kamati ya Ulinzi na Usalama kufika hapo siku hiyo ya Jumamosi ili kujiridhisha kama kazi inaendelea.
Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mlele, Mhandisi Gilbert Isack alisema mradi huo wa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2 ulianza kutekelezwa mwaka 2018 na ulipaswa kukamilika mwaka 2019.
Mhandisi Isack alisema kukamilika kwa mradi huo kutatosheleza mahitaji ya wananchi wa vijiji hivyo 16 kwani mahitaji kwa sasa ni takribani lita milioni 500 kwa mwaka wakati bwawa hilo uwezo wake ni kuhifadhi zaidi ya lita bilioni 2 kwa mwaka.