WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahakikishia wakazi wanaohama kwa hiari yao kutoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga kuwa hakuna shughuli zao zitakazosimama na kwamba wataendelea na ufugaji katika mazingira bora zaidi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya wananchi waliokuwa wakiishi katika Hifadhi ya Ngorongoro ambao wamekubali kwa hiari yao kuhamia katika kijiji cha Msomera wilayani Handeni wakati aliposhuhudia awamu ya pili kuhama kwao katika Ofisi Kuu ya Hifadhi ya Ngorongoro Mkoani Arusha, Juni 23, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………….
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 23, 2022) wakati akiwaaga wakazi wa Ngorongoro wanaohama kwa hiari yao kwenda kijiji cha Msomera na kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo hilo. Hii ni awamu ya pili ya wakazi wanaohama katika eneo hilo kuelekea Msomera. Mazungumzo hayo yamefanyika kwenye viwanja vya Ofisi Kuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCCA), Ngorongoro mkoani Arusha.
Waziri Mkuu ambaye ameshuhudia wakazi hao takribani 127 kutoka katika kaya 27 wakihama na kuelekea kijiji cha Msomera, amewapongeza kwa uamuzi huo na kuwahakikishia kwamba Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwapa ushirikiano.
Amesema uamuzi walioufanya wa kuhamia Msomera na kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo la Ngorongoro ni uamizi sahihi, hivyo ametumia fursa hiyo kuwahakikishia kwamba hakuna shughuli zao zozote zitakazisimama, wataendelea na ufugaji kwa kuwa Msomera kuna eneo kubwa na la kutosha.
“Ninawaomba msafiri kwa amani kabisa na mioyo yenu ikunjuke. Isikilizeni Serikali yenu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Sasa hivi mko huru, nenda mkakae kwenye nchi yenu kwa uhuru,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dkt. Christopher Timbuka amesema awamu ya pili ya zoezi la kuwahamisha wakazi wa eneo la Ngorongoro kwa hiari lilianza Juni 20, 2022, ambapo inahusisha jumla ya kaya 27 zenye watu 127 na mifugo 488. Aidha kaya moja kati ya hizo itahamia Karatu.
Dkt. Timbuka amesema hadi sasa kaya zilizohama kwa hiari katika eneo la Ngorongoro katika awamu ya kwanza na ya pili ni 48 zenye jumla ya watu 233 na mifugo 899. Amesema utaratibu wa kuwahamisha umefanyika kwa kufuata hatua mbalimbali ikiwemo kuhakiki idadi ya watu.
Pia, hatua nyingine ni kusainisha vitabu vya fidia vya wakazi wanaohama kwa hiari awamu ya pili, kuhakiki idadi ya mifugo na kuiweka alama ili iweze kusafirishwa pamoja na kuhakiki na kutambua aina za nyumba za wakazi hao kwa ajili ya taratibu za ubomoaji.
Dkt. Timbuka amesema mbali na kupewa nyumba, fidia na shamba kaya zote pia zitapewa magunia mawili ya mahindi kwa kwa kipindi cha miezi mitatu ili waweze kujikimu katika kipindi cha mpito wakati wakijiandaa na msimu wa kilimo.
Naye, mmoja wa wakazi hao wanaohama kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, Bw. Emmanuel Saitoti kutoka kijiji cha Nainokanona ameishukuru Serikali kwa upendeleo ilioutoa kwao kwa kuwa mbali ya kupewa nyumba pia Msomera wanakwenda kupata fursa zitakazowaongezea tija kiuchumi.
“Serikali tunaishukuru imetupendelea sana, tumepata hati za nyumba na mashamba pamoja fidia ya fedha, naishauri iendelee kuwahamasisha na wakazi wengine nao wahame kule hakuna maendeleo. Msomera tunakwenda kufanya shughuli nyingi za maendeleo.”