Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akifungua Mkutano wa kumi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha Kanda ya Afrika kwa njia ya Mtandao unaofanyika jijini Arusha akiwa jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)
…………………………………………..
Na. Peter Haule, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kuwa thamani ya miamala ya simu katika pato la Taifa (GDP) imepanda kutoka asilimia 40 kwa mwaka 2013 hadi asilimia 66 kwa mwaka 2021.
Dkt. Nchemba amebainisha hayo wakati akifungua Mkutano wa kumi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha Kanda ya Afrika kwa njia ya Mtandao unaofanyika jijini Arusha kwa siku tatu.
Dkt. Nchemba aliyefungua mkutano huo kwa njia ya mtandao akiwa Dodoma alisema kuwa Tanzania ina mengi ya kuelezea kuhusu teknolojia ya kidigitali katika kuchochea huduma jumuishi za fedha na maendeleo ya uchumi kwa kuwa utafiti uliofanywa mwaka 2013 na 2017 wananchi waliopata huduma rasmi za fedha walikuwa asilimia 57 na 65 wakati mwaka 2006 wananchi walitumia huduma hiyo rasmi walikuwa asilimia 11.
“ Serikali ilitengeneza mazingira wezeshi ya huduma za kifedha na kuruhusu huduma hizo kwa njia za simu za mkononi kwa kushirikiana na Benki jambo lililoongeza wigo wa huduma za fedha na kupunguza gharama za miamala”, alieleza Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa watumiaji wa miamala kwa njia ya simu wawamefikia milioni 35.3 hadi Desemba 2021 ikiwa ni asilimia 61 ya jumla ya idadi ya watanzania.
Alisema kuwa miaka ya nyuma changamoto zilizosababisha kuwa na watumiaji wachache wa huduma za fedha ni pamoja maeneo mengi kutofikika kwa urahisi hususani ya vijijini na gharama kubwa za huduma za kibenki.
Aidha Dkt. Nchemba, aaliwapongeza wajumbe wa mkutano kwa kuweka utaratibu wa kufanya mikutano kila mwaka ili kujadili huduma jumuishi za fedha katika Kanda ya Afrika.
Waziri Nchemba ametumia jukwaa hilo kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza Tanzania na kuwaahidi kutoa ushirikiano kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mkutano huo ambao mwenyeji wake ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, umewakutanisha Magavana, Manaibu Gavana na wageni wengine.