Home Mchanganyiko WATUMISHI WIZARA YA UTAMADUNI WAHIMIZWA KUFANYA KAZI KWA BIDII

WATUMISHI WIZARA YA UTAMADUNI WAHIMIZWA KUFANYA KAZI KWA BIDII

0

Na Shamimu Nyaki  – WUSM, DODOMA

Watumishi  wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wamehimizwa kufanya kazi kwa bidii na kulinda amani,  utamaduni wa mtanzania na kudumisha uzalendo kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utawala na Rasilimali Watu Bibi. Zahra Guga, katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Juni 23, 2022 Jijini Dodoma.

“Tufanye kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma, Wizara yetu ni miongoni mwa wizara ambazo Sekta zake zinachangia kwa kiasi kikubwa katika Pato la Taifa kupitia ajira za wadau wake”alisema Bi. Zahra.

Ameongeza kuwa  wizara hiyo ni  nguvu shawishi ya nchi katika kukuza uchumi hivyo watumishi wanapaswa kuzingatia hilo katika utendaji wao kwa kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake ipasavyo kwa kufuata Kanuni, miongozi na taratibu za Serikali, huku wakijielekeza katika kushawishi na kutenda mazuri nje ya maeneo ya kazi.

Kwa upande wake Afisa Michezo wa wizara hiyo, Rashidi Mijuza amesema kuwa wizara imefanya jambo jema kuadhimisha wiki hiyo kwa kutembelea jamii ambazo zina uhitaji pamoja na wadau ambao wanaunga mkono juhudi za wizara katika kukuza michezo, utamaduni na Sanaa.