Kiongozi wa mbio za mwenge , Sahil Geraruma akipata maelekezo kuhusu bidhaa hizo zitokanazo na asali kutoka kwa Mwenyekiti wa kampuni ya Sessan Enterprises Ltd, Emmanuel Msafiri (mwenye tisheti nyeupe)
Mwenyekiti wa kiwanda cha Sessan Enterprises Ltd cha kuchakata mazao ya asali , Emmanuel Msafiri akizungumza kuhusiana na shughuli wanazofanya mara baada ya mwenge wa Uhuru kuzindua kiwanda hicho jijini Arusha.
………………………………
Julieth Laizer ,Arusha
Arusha.Mwenge wa Uhuru umezindua kiwanda cha kuchakata na kuzalisha asali kilichopo eneo la Themi Njiro ambacho kimeweza kutoa ajira kwa vijana ambao wameweza kujiajiri na kuondokana na changamoto mbalimbali.
Aidha kiwanda hicho ni miongoni mwa kiwanda kilichopatiwa mkopo wa asilimia 10 na halmashauri ya jiji la Arusha kwa ajili ya kukiboresha na kuongeza uzalishaji ambapo walipatiwa kiasi cha shs 30 milioni.
Akizungumza katika uzinduzi huo jijini Arusha ,Mwenyekiti wa kiwanda hicho cha Sessan Enterprises , Emmanuel Msafiri amesema kuwa, kiwanda hicho kilianza mwaka 2021 ambapo kimekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kutoa ajira kwa vijana zaidi ya 30 na gharama ya mradi huo hadi kukamilika ni shs 36.5 milioni.
Amesema kuwa, fedha hizo walizopatiwa na halmashauri zimeweza kuwasaidia kununua mashine ya uchakataji na kuongeza malighafi za uzalishaji wa bidhaa hizo zitokanazo na asali.
“Namshukuru Sana Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ametoa maelekezo kwa halmashauri kutoa mikopo hiyo ya asilimia 10 kwa ajili ya vijana,walemavu na wanawake ambapo imetusaidia sisi kuongeza uzalishaji kiwandani hapa na kuweza kuongeza ajira zaidi.”amesema.
Amesema kuwa, mbali na kuzalisha asali hiyo wamekuwa wakitumia kiwanda hicho kama kituo kwa ajili ya kutoa elimu ya ufugaji nyuki kwa vijana ambapo elimu hiyo imeweza kuwasaidia vijana wengi kuweza kujiajiri kwa kuanzisha miradi yao ya nyuki na kuweza kujikwamia kiuchumi.
Msafiri amesema kuwa, wamekuwa wakizalisha bidhaa bora za lishe na afya ya mwili na ngozi zilizotengenezwa kwa kutumia mazao ya nyuki ikiwemo mafuta ya ngozi,mafuta ya watoto,losheni ya ngozi,sabuni ya kuogea na utoaji wa mafunzo ya nyuki.
Naye Kiongozi wa mbio za mwenge ,Sahil Geraruma amesema kuwa, ameridhishwa na mradi huo kwa namna unavyofanya kazi na kutoa ajira kwa vijana ambao nao wameweza kuwaajiri vijana wengine na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira.
“Nimeridhishwa sana na mradi huu na nimeona namna ambavyo zile asilimia 10 zilivyotumika vizuri ,na naomba halmashauri iendelee kuwapatia mikopo zaidi ili waweze kuendeleza kiwanda hiki na kutoa ajira zaidi kwa makundi ya vijana ambao wengi wao wanakaa mitaani bila kazi yoyote.”amesema.
Sahil amewataka wale wote wanaonufika na mikopo hiyo kujitahidi kurejesha kwa wakati ili na wengine waweze kunufaika na fursa hiyo kwani namna ambavyo watajitahidi kurejesha ndivyo na idadi ya wanufaika itakuwa kubwa.