Muogeleaji wa klabu ya FKBlue Marlins, Lorita Borega akishindana katika mashindano yaliyopita.
……………………………………..
Jumla ya klabu tisa za mchezo wa kuogelea zimethibitisha kushiriki katika mashindano ya waogeleaji chipukizi (Junior Championships) yaliyopangwa kufanyika kwenye bwawa la kuogelea la Shaaban Robert jijini Julai 2 na 3.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA), Hadija Shebe amezitaja klabu hizo kuwa ni Bluefins, Champion Rise, FK Blue Marlins, Lake swimming club, MIS Piranhas, Mwanza Swim Club, Pigec, Dar es Salaam Swimming Club na Taliss-IST .
Hadija alisema kuwa maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea vizuri na waogeleaji wanajifua vilivyo ili kuweza kushinda medali, vikombe na kuboresha muda wao wa kuogelea.
Alisema kuwa kampuni ya Kilombero Sugar Company Limited ndiyo wadhamini wakuu wa mashindano hayo huku Burger 53, Rap & Roll, Pepsi na F & L Juice ni wadhamini wasaidizi.
Kwa mujibu wa Hadija, mashindano hayo yatashirikisha waogeleaji chipukizi kuanzia miaka 12 kushuka chini na yana lengo la kuibua vipaji vya waogeleaji kwa ajili ya kushiriki mashindano makubwa na ya kimataifa.
“Tunawaomba wadhamini wengine wajitokeze ili kufanikisha mashindano haya muhimu kwa maendeleo ya mchezo wa kuogelea nchini. Kuna gharama mbalimbali ikiwa pamoja na uendeshaji wa mashindano pia, siyo kazi rahisi kufanywa na TSA, tunaomba wadau wasaidie,” alisema Hadija.
Alisema kuwa kila klabu inatakiwa kuorodhesha majina ya waogeleaji wake wakiwa na umri na aina ya mashindano ambayo wanatakiwa kushindana ili kuwawezesha kuandaa programu kamili ya mashindano hayo.
“Mashindano haya yatatoa fursa kwa waogeleaji ambao walishindwa kushindana katika mashindano ya wakubwa kutokana na kigezo cha umri, kwa vile TSA inatambua waogeleaji chipukizi, tumeamua kuandaa mashindano ambao yatawafanya waogeleaji wanaochipukia nao kujipima uwezo wao,”alisema.
Alisema kuwa kutakuwa na makundi manne, kundi la waogeleaji waliochini ya miaka saba, waogeleaji wa miaka nane na tisa, 10 na 11 na 12. Washindi wa jumla katika kila kundi atazawadiwa kikombe wakati washindi wa kila shindano watapata medali.