*Kikao
kazi hiki kimejenga uelewa mkubwa kwa maafisa habari
*Tutaendelea
kutoa elimu zaidi kuhusu Fidia zitolewazo na WCF
NA MWANDISHI WETU
Mkurugenzi
Mkuu wa Idara ya Habari -MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa
ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa kutoa huduma bora kwa
wafanyakazi wanaopata ajali wakiwa kazini.
“Tunashukuru
kwa Mkurugenzi Mkuu na timu nzima ya WCF, kwa kuandaa kikao kazi muhimu kwani imekuwa
nafasi muafaka ya kufuatilia taarifa kama maafisa habari katika utendaji kazi
wetu wa kuisemea serikali, pia imetusaidia kuongeza uelewa wa masuala
mbalimbali kuhusu fidia kwa wafanyakazi” alisema Bw. Msigwa.
Akizungumza
katika kikao kazi hicho, Bw. Msigwa amesema serikali imefanya kazi kubwa
kuhakikisha WCF inakuwa imara kama Mfuko wenye jukumu la kufidia Wafanyakazi na
tangu kuanzishwa kwake WCF imeendelea kutoa fidia kwa wafanyakazi wanaopata
matatizo yanayotokana na kazi.
“Tumeweza
kujua sheria iliyounda WCF na jinsi inavyofanya kazi, pia tunakazi kubwa ya
kuelimisha jamii na watanzania juu ya nini wanatakiwa wakipate kutoka WCF”
alifafanua Bw. Msigwa.
Katika
kuboresha mazingira ya biashara na kuwezesha waajiri kuwasilisha michango kwa
wakati, Serikali imeweza kupunguza kiwango cha michango kutoka asilimia 1 hadi
asilimia 0.6 kwa Sekta Binafsi, lengo lingine likiwa kuwapa utulivu wafanyakazi
endapo wakipata changamoto kutokana na kazi kwa kupata amani ya kulipwa fidia.
‘Nitoe
wito kwa waajiri wote tulete michango kadiri inavyotakiwa. Tunajua wengi
mnawasilisha lakini tuendelee ili tuweze kuwahudumia Wafanyakazi maana sio
rahisi kujua ni wakati gani utapata madhara ukiwa kazini ama kupata maradhi ukiwa
kazini. Mwajiri unapotoa michango ya
Wafanyakazi wako inavyotakiwa unafanya mfanyakazi kufanya kazi akiwa na amani akijua
inapotokea tatizo lolote basi WCF ipo kwa ajili yake na hiki ndio tungependa
waajiri wote wakitekeleze.
Niwapongeze
Waajiri wote mnaowasilisha michango yenu WCF, na ambao hamfanyi hivyo basi
muwasilishe michango hiyo WCF kwa wakati.
“Tanzania
ni moja ya nchi chache barani Afrika kama sio duniani zenye Mfuko madhubuti wa
Fidia kwa wafanyakazi ambao unafanya kazi vizuri ndio maana Shirika la Kazi
Duniani -ILO limethibitisha kuwa WCF inaweza kutoa huduma zake mpaka 2048 hilo
ni jambo kubwa sana kwa Wafanyakazi, wa kuwa na uhakika wana Mfuko imara wa
kuwahudumia kwa muda mrefu” alisema Bw. Msigwa
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma akizungumza wakati wa kikao
kazi hicho alisema ni muhimu sana kwa waajiri kuwachangia watumishi wao ili
waweze kupata fidia pindi wanapoumia wakiwa kazini.
Kikao
kazi hicho kimekutanisha watendaji kutoka ofisi ya Msemaji Mkuu wa serikali ambaye
pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo na watendaji wa Mfuko wa Fidia
kwa Wafanyakazi – WCF.