…………………….
Wahifadhi wametakiwa kusimamia vyema sheria za uhifadhi ili kukabiliana na baadhi ya watu wachache wanaofanya uharibifu katika maeneo ya Hifadhi nchini.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito huo mkoani Njombe, alipokuwa akizungumza na Maafisa Uhifadhi wa Kanda ya Kusini.
Amesema wapo watu wachache wanaovunja sheria za uhifadhi kwa makusudi na wengine kwa kutokujua sheria, hasa wafugaji wanao ingiza mifugo kwenye Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba yaliyo kwenye Kanda hiyo ya Kusini na kusisitiza kuwa sheria zilizopo zisipo simamiwa kikamilifu madhara yatakuwa makubwa sio tu kupoteza sifa za hifadhi hizo bali kupunguza idadi ya watalii ambao wamekuwa chanzo kikubwa na mapato ya nchi.
Awali akiwasilisha taarifa za utekeleza wa majukumu na hali ya uhifadhi wa Pori la Akiba la Mpanga Kipengere, Mhifadhi Mwandamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Alfred Kipondamali amesema moja ya mafanikio yaliyopatikana ni kusaidia jamii inayo zungula pori hilo kwa kuchangia vifaa vya ujenzi wa shule na kituo cha Afya katika Kijiji cha Mpangampya
Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Kitulo inayosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Theodera Aloyce amewashauri Madiwani wa Mkoa wa Njombe kushirikiana na Taasisi hiyo hasa katika kuchangamkia fursa zitokanazo na Utalii Kanda ya Kusini katika kutoa huduma kwa watalii kutokana na Matokeo chanya ya Filamu ya Royal Tour.
Naye Afisa Misitu Wilaya ya Njombe, Bw Audatus Kashamatula akiwasilisha taarifa ya mkoa huo katika suala la uhifadhi amemweleza Waziri Chana changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ambazo ni pamoja na vitendo vya uvunaji wa miti michanga, uchomaji wa moto, kasi ndogo ya upandaji miti na viwanda vichache vya uchakataji wa mazao ya misitu
Mhe. Waziri Chana yupo mkoani Njombe kwa ziara ya kikazi ya kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za uhifadhi katika Kanda ya Kusini.