Katibu Mkuu ametoa onyo kwa makatibu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa kujihusisha na makundi ya wagombea katika uchaguzi unaoendelea ndani ya Chama na jumuiya zake.
Katibu Mkuu ameeleza hayo akiwa mgeni rasmi katika kikao cha kawaida cha Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania Makao Makuu ya Chama Dodoma leo Jumatano tarehe 15 Juni, 2022.
“Nitoe Onyo kwa Makatibu wa Jumuiya, najua tangu mmeingia Dodoma mnazungushwa tu na wagombea, habari ninazo, kwa kuona, kwa ushahidi, na kila kitu mnazungushwa kutoka hoteli moja kwenda nyingine.”
Ndg. Chongolo amesistiza kuwa “Narudia natoa onyo kwa makatibu wote nchini, ninyi ni wakurugenzi wa uchaguzi, sitamani wala nisingependa kuona mnalichukulia suala hili la uchaguzi kishabiki kwa kutengeneza wagombea, nawaasa, kazi ni nzuri ukiikosa lakini ni mbaya sana ukiwa nayo.”
Na kwa bahati mbaya hao mnaowahangaikia hawana uwezo wa kuwarudisha kazini, siku moja kazi ukiikosa.