…………………
Adeladius Makwega-DODOMA.
Msomaji wangu, leo hii nakuletea picha hiyo juu ya ndugu zangu wanne; Biligita (57),Demetria (52), Bernadeth (56) na Corinelia (amefariki) wote ni Binti Makwega iliyopigwa mwaka 1985 Mbagala Sabasaba Temeke-Dar es Salaam wakiwa mabinti wadogo sasa ni watu wazima.
Mimi siku hiyo sikuwepo lakini kwa desturi ya maisha yetu ya Tanzania ya wakati huo picha zilipigwa sana wakati wa wa sikukuu tu, sivyo kama ilivyo sasa, kwa kuwa wapiga picha walipata wasaa wa kupata wateja wengi siku za sikukuu kuliko siku nyengine yoyote.
Ndugu zangu hao wote walisoma shule ya msingi Mbagala tangu darasa la kwanza hadi la saba na mimi nikiwashuhudia wakisoma shule hii kongwe ya msingi.
Umbali kati ya nyumbani kwetu na shule hii ni kama kilomita tatu. Wakipita njia ya Bonde la shamba la Jaji Mstaafu Kimicha ambalo aliuliziwa na Bibi Sela (Bibi Sara) Bibi mmoja mzungu ambaye aliondoka kurudi kwao ughaibuni muda mfupi baada ya uhuru Tanganyika.
Kwa hiyo shule ya msingi Mbagala ukijumlisha waliosoma wengi kutoka kwetu baba, mashangazi zangu hao, sisi watoto wao wote wa kike na wakiume, tulikuwa wengi mno idadi inakaribia kati ya watu 20-30 wa ukoo mmoja kwa kipindi cha mfuatano tafauti tangu mwaka 1950 na hadi sasa ikiongezeka zaidi.
Zipo koo zingine nyingi kama vile Zame, Makuka, Mkundi(Kizuiani), Mkundi(Sabasaba), Linje, Ngunga, Ungaunga na Mangaya zikiungana na akina Makwega wakisoma wengi shuleni hapo, huku zikiwepo koo nyingine nyingi zilizokuwa na watu wachache wachache shuleni.
Tukiwa tunakwenda shuleni tuliongozana makundi makundi, yawe ya watu watano watano huku wale wadogo wakiongozwa na waliokuwa wakubwa iwe wakati wa kwenda shuleni au wakati wa kurudi nyumbani.