WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe leo Jumatatu- Mei 16 amekutana na Maafisa Kilimo kutoka mikoa 26 nchini na kuwapatia mikakati ya wizara ambayo maafisa hao wanatakiwa kwenda kuitekeleza katika mikoa yao.
Bashe amesema serikali imejipanga kukiongezea thamani kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 na kuwataka maafisa hao kutambua kuwa wanajukumu kubwa la kuhakikisha ndoto hiyo inafikiwa
Amesema ili kuhakikisha lengo linatimia serikali imeamua kutatua changamoto za maafisa hao kwa asilimia 100 na kutaja kati ya hatua iliyochukua ni pamoja na kuwapatia pikipiki 7,000 ambazo zimefungwa mfumo wa ufuatiliaji utakaowezesha kujua pikipiki ipo wapi na kwa muda gani.
Pia amebainisha, kila Afisa Ugani atapatiwa kompyuta ndogo ya mkononi kwa ajili ya kurekodi taarifa za wakulima watakaotembelewa na pia maafisa hao wote watapatiwa mafuzo maalumu ya nidhamu na uwajibikaji kutoka Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).
Amesema serikali inataka kuhakikisha maafisa kilimo wawe ni kama wanajeshi wenye kukipigania kilimo na kusisitiza kuwa wizara yake itapigania maslahi ya maafisa kilimo kwa kuhakikisha wanapatia heshima stahiki katika ngazi za kilimo.
“Najua nyie maafisa kilimo ni mashujaa wenye jukumu la kuchagiza ile nia ya serikali ya kukifanya kilimo kuwa na tija kubwa zaidi kwa nchi, yani tuuze mazao ya kilimo nje ya nchi na kuvuna fedha nyingi zaidi za kigeni kutoka Dola za Marekani bilioni 1.2 hadi kufikia bilioni tano na kuchangia zaidi katika pato la taifa”
Amesema, lengo ni kuhakikisha kufikia mwaka 2025 upimaji wa Afya ya udongo ufike kwenye kata 4,000 nchini na wakulima watapatiwa cheti cha upimaji wa Afya ya udongo ili walime kwa ufanisi zaidi hatua itakayoongeza kiwango cha mazao sokoni, hivyo maafisa kilimo wanapaswa kujipanga kuelimisha.
Alisema kuwa serikali imekuwa ikitumia Sh bilioni 500 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi na mwaka huu walifanya majaribio ya kugawa tani 2,000 ya mbegu za alizeti na kwa mwaka ujao wa fedha ina mpango wa kugawa tani 5,000 za zao hilo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa kilimo Antony Mavunde ametaka ushirikiano wa pamoja Ili kufikia malengo yaliyowekwa na kuwahakikishia maofisa ugani hao kuwa wanaongeza ubunifu zaidi katika utendaji kazi wao.
Pia Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Andrew Massawe alisema mkutano huo umehusisha maafisa ugani mikoa 26 ambapo idadi yao ni 210 kati yao 26 wakiwa ni wawakilishi wa mikoa na 184 wa Halmashauri.
Alisema katika mwaka huu wa fedha wametoa mafunzo 2,886 kwa maafisa ugani na Wakulima viongozi 870.