BENKI ya NMB imezinduwa rasmi Kampeni ya Teleza Kidijitali, ambayo imelenga kuwaelimisha Watanzania umuhimu wa kutumia na kunufaika na huduma zilizo chini ya kampeni hiyo za NMB Pesa Wakala, Lipa Mkononi na Mshiko Fasta.
Kampeni hiyo imezinduliwa jijini Dar es Salaam katika Tawi la Benki ya NMB Tandika, ambapo Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna, akiwa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Bw. Filbert Mponzi na Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo waliwatembelea wafanyabiashara madukani mara baada ya tukio hilo kuwapa elimu zaidi.
Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya NMB wakitoa huduma mitaani kwa wateja mara baada ya uzinduzi wa huduma hiyo. |
Akizungumza na wanahabari mara baada ya uzinduzi, Bi. Zaipuna alisema NMB imelenga kutoa elimu ya kutosha na kuwaingiza Watanzania wengi zaidi kwenye sekta rasmi ya kifedha ili waweze kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa.
“Tuko hapa kunadi huduma zote muhimu zilizopo kwenye mwamvuli wa Teleza Kidijitali, ikiwa ni ufunguaji wa akaunti za NMB, Mshiko Fasta ambapo mteja anaweza kupata mikopo nafuu isiyo na dhamana kupitia simu yake tu.”
“Pia tumeutumia uzinduzi wa kampeni hii kwa ujumla kunadi huduma ya Lipa Mkononi, ambayo itamuwezesha mfanyabiashara kulipwa na wateja wake kwa kutumia lipa namba au kwa kuskani QR, huku ikitupa sisi kumbukumbu na historia ya mfanyabiashara huyo, kutusaidia hata katika utoaji wa mikopo.
“Pia tumekuja na NMB Pesa Wakala, huduma inayomuwezesha mtu yeyote kuwa wakala kwa kupitia simu yako ya mkononi (smart phone au tochi) kutoa huduma za kuweka, kutoa au kutuma pesa kirahisi,” alisema Zaipuna, ambaye alishiriki kutembelea wafanyabiashara wa eneo la Tandika madukani mwao kutoa elimu na kusikiliza maoni yao.
Kwa upande wake, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, aliwataka wakazi wa kanda yake kuchangamkia fursa zilizomo ndani ya kampeni hiyo, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bila kusumbuka kwenda matawini.
Huduma ikitolewa mitaani mara baada ya uzinduzi wa kampeni hizo. |