Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Furahika Education Dkt. David Msuya akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
…………………
Watanzania wametakiwa kuchangamkia fursa ya kujiunga na mafunzo ya kozi Uuguzi (Nursing) ngazi ya cheti yanayotolewa bure bila gharama yoyote na Chuo Furahika Education Tanzania kilichopo Buguruni jijini Dar es Salaam kupitia mradi wa Msaidie Mama Mjamzito
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Furahika Education Dkt. David Msuya, amesema mwisho wa kutuma maombi tarehe 18/5/2022 kwa ajili ya kujiunga kozi ya uuguzi inayotolewa bure na chuo hicho.
Dkt. Msuya amesema kuwa lengo ni kuwafikia vijana wote wa kitanzania na kuwapa elimu, kwani kila mwaka katika kozi ya uuguzi wanatarajia kuchukua wanafunzi 200.
“Sifa ya wanafunzi ili ajiunge na kozi ya uuguzi lazima awe amepata Biology alama D au C, na mafunzo yanatarajia kuanza mwezi huu tano mwaka 2022” amesema Dkt. Msuya.
Ameeleza kuwa mradi wa Msaidie Mama Mjamzito utachukua wanafunzi 100 baada ya kumaliza masomo ya uuguzi kwa muda wa mwaka mmoja ambapo watakwenda kufanya kazi katika vituo mbalimbali watakavyopangiwa.
“Wanafunzi wanapokuja kujiunga waje na barua ya utambulisho kutoka Mwenyekiti wa serikali za mtaa unapoishi” amesema Dkt. Msuya.
Amefafanua kuwa wazazi wanatakiwa kuchangamkia fursa ya kuwapa elimu vijana wao, kwani itawasaidia katika maisha na kupiga hatau katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.
“Sisi tunatoa mafunzo bure bila kulipa ada, wanafunzi anachangia gharama ya ndogo sh. 20,000 kwa ajili ya kulipa ada za mtihani, na tunatoa huduma za hosteli bure lengo ni kuwasaidia vijana wa kitanzania wapate elimu, kuna watu wanatumia fedha nyingi kuwapa elimu watoto wao” amesema Dkt. Msuya.
Chuo cha Furahika Education kimesajili na VETA na wanatoa kozi mbalimbali bure bila kulipa ada, hivyo wananfunzi wanachangia ada ya mitihani wanayofanya ili waweze kupata cheti.
Lengo la Chuo ni kuwaendeleza kielimu watoto wa kike na vijana kuwapa ujuzi mbalimbali kwaajili ya mafanikio yao na familia kwa ujumla.
Katika hatua nyengine amempongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Mjaliwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kuwatumia watanzania na kuleta maendeleo kwa Taifa la Tanzania.