WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa akifungua mkutano wa Serikali na viongozi wa kimila nchini kushiriki kikamilifu katika sensa ya watu na makazi kwa kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki kwenye sensa ya mwaka huu mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Julius Nyerere Posta.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022, Anna Makinda akizungumza katika mkutano wa Serikali na viongozi wa kimila nchini kushiriki kikamilifu katika sensa ya watu na makazi kwa kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki kwenye sensa ya mwaka huu
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa akishiriki katika mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Julius Nyerere Posta.
Picha mbalimbali zikionesha baadhi ya machifu wakiwa kwenye mkutano huo.
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amewataka machifu pamoja na viongozi wa kimila nchini kushiriki kikamilifu katika sensa ya watu na makazi kwa kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki kwenye sensa ya mwaka huu.
Amesema kutokana na nguvu ya ushawishi waliyonayo viongozi hao kwa wananchi ni wazi kuwa wanao uwezo wa kuwashawishi wananchi kushiriki kikamilifu kwenye sense ya mwaka huu huku akiwataka kutoa taarifa kwa serikali kama kutakuwa na vikwazo vyovyote vitakavyojitokeza wakiwa kwenye utendaji kazi wao.
Mchengerwa ametoa rai hiyo leo katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa kwa Julius Nyerere(JNICC) na kuhudhuriwa na machifu na viongozi wa mila kutoka mikoa mbalimbali nchini pamoja na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Tanzania Bara, Anna Makinda na Kamisaa mwenzake kutoka serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Balozi Mohamed Haji Hamza.
“Serikali inatambua kwa kiasi kikubwa uwezo wenu katika kufanikisha sensa ya watu na makazi mwaka huu na ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan alitaka ushiriki wenu kikamilifu kwenye mchakato huu wa sensa ya mwaka huu na niwahakikishie kuwa serikali itaendelea kuwashirikisha kwenye masuala mbalimbali yanayohitaji ushiriki wenu.’’ amesema Mchengerwa.
Naye Anna Makinda aliwataka makarani wa sensa kuwahesabu watu wote kuanzia watoto wachanga watakaozaliwa siku moja kabla ya siku ya sensa ambayo ni Agost 23 pamoja na watu wengine wote wakiwemo wenye ulemavu pamoja na watu wanaoishi kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo hospitali, nyumba za kulala wageni hadi watoto wanalala mitaani.