Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Balozi Dkt Pindi Chana (picha na maktaba)
……………………
Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Balozi Dkt Pindi Chana ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania –TAWA kwa kutenga maeneo ya uwekezaji katika eneo la masuala ya wanyamapori ili kuendelea kuwavutia watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Waziri Dkt Pindi Chana ametoa kauli hiyo mkoani Morogoro wakati alipofanya ziara kwenye ofisi za Mamlaka hiyo kwa lengo la kufanya ukaguzi na kujionea maendeleo ya maeneo hayo ikiwa ni siku chache kufuatia Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluh Hassan kuzindua Filamu ya Royal Tour.
Balozi Dkt Chana amesema Tanzania imesheheni vivutio vingi zikiwemo Hifadhi,Fukwe,mapori ya akiba,mapori yanayomilikiwa na vijiji hivyo kupitia Filamu ya Royal Tour inaonyesha Tanzania kuwa ni sehemu nzuri ya kufanya utalii pamoja na uwekezaji.
Aidha Waziri Dkt Chana amesema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake ikiwemo TANAPA,TAWA,na maeneo mengine ya utalii imejipanga katika maeneo mbalimbali kuhakikisha wanawavutia watalii kuja kuwekeza nchini.
Akizungumza kuhusiana na utalii Waziri Dkt Chana amesema unachangia asilimia 17 ya pato la Taifa lakini pia unasaidia kuongeza ajira wa kwa Watanzania hivyo Royal Tour inakumbusha taratibu kwa wageni wanapokuja kufanyika kwa haraka.
Awali akizungumza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania –TAWA Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko amemshukuru Waziri Dkt Chana kwa kufanya ziara katika Taasisi hiyo kwani itasaidia kuwajenga zaidi.
Hata hivyo Waziri Balozi Dkt Pindi Chana amewataka wawekezaji kutumia fursa kuwekeza katika utalii kwani milango ipo wazi.