Na Dotto Mwaibale, Singida
KAMATI ya Ulinzi na Usalama wilayani Ikungi ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Wlaya hiyo Jerry Muro imetembelea na kukagua Msitu wa Asili wa Minyughe ili kujionea changamoto mbalimbali zinazotishia kutoweka kwa msitu huo.
Katika ziara hiyo kamati hiyo ilitembelea taasisi za Serikali zilizojengwa katika msitu huo hasa shule na kujionea tishio kubwa la kutoweka kwa msitu huo kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu kama kilimo, ufugaji, ukataji miti kwa ajili ya kuchoma mkaa na kuanzisha makazi.
Shule walizozitembelea ni Shule ya Msingi Mkenene,Shule Shikizi ya Ilowoko, Shule Shikizi ya Munyu na Maghwagana ambapo pia katika maeneo hayo kuna makazi ya watu ya kudumu yalioanzishwa.
Akizungumza katika ziara hiyo iliyofanyika juzi ikiwahusisha viongozi waandamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani humo, mkuu wa wilaya hiyo, Jerry Muro alisema lengo la ziara hiyo ni kujiridhisha kabla ya hatua ya kuukabidhi msitu huo kwa TFS ambao wanauwezo mkubwa wa kuusimamia kutokana na umuhimu wake.
Alisema ziara ya namna hiyo ni ya nne na kuwa sasa wapo kwenye hatua ya mwisho ya kutumia busara na hekima ya namna gani wanaweza kuielimisha jamii iliyopo ndani ya msitu huo na kuzungumza nayo na wale waliopo mbembezo ili kwa pamoja waone ni njia gani ya maisha ifanyike ya kuendelea kuwepo ndani ya msitu huo bila ya kuuathiri na msitu kuwepo bila ya kuathiri maisha ya wananchi.
“Hiki ndicho tunacho kifanya leo na ni lazima tujiridhishe na kuona hali ikoje na sisi kama Serikali tunaweza kufanya nini kunusuru msitu huu wa Minyughe na nyinyi mmeona wapo watu wanalima, wanakata miti, wanafanya shughuli za kijamii hivyo ni lazima kuhifadhi msitu” alisema Muro.
Akitolea mfano wa majengo ya taasisi za Serikali alisema kuna Shule Shikizi ya Ilowoko ambayo zamani ilikuwa na madarasa mawili lakini baada ya kupata fedha Sh.Bioni 2.6 ndipo walipojenga madarasa manne na ofisi mbili za walimu hivyo kuboresha maisha ya wanafunzi na kuongeza thamani ya maisha ambapo kutoka makuu ya wilaya hadi kufika katika shule hiyo ni takribani kilometa 120 lakini wao hawakuangalia umbali bali kuboresha shule ambazo ziko pembezoni kabisa ya wilaya hiyo lakini changamoto kubwa ikiwa ni shule hiyo ipo ndani ya hifadhi ya msitu.