MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana ametoa ushauri kwa Serikali kuhakikisha wote waliotajwa kufuja fedha za umma kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG) wanachukuliwa hatua.
Amesema haina maana kila mwaka ripoti ya CAG inatolewa halafu hakuna hatua ambazo zinachukuliwa dhidi ya wahusika wote ambao wametajwa, hivyo umefika wakati sasa kuchukua hatua ili kukomesha ufujaji wa fedha za umma.
“Kumekuwa na matumizi mabaya ya fedha za umma kinyume na utaratibu, niwoambe wenzangu serikali, ni wakati muafaka watu waliotajwa, waliohusika, waliotenda, walioshiriki kwa namna moja au nyingine wachukuliwe hatua.
“Wakati umefika kwa Serikali kufanyia kazi kwa kina ripoti ya CAG ili wananchi waridhike mali ya umma haitumiki vibaya.Mnaunga mkono au tuwahurumie, haiwezekani vitabu vya CAG vinaandikwa kila mwaka hali inakuwa hivyo hivyo , lazima tuchukue hatua, uamuzi wa kuagiza serikali sina lakini uwezo wa kushauri ninao,”amesema Kinana.