Mkugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na washiriki wa mafunzo ya mwezi mmoja ya kufanya uchunguzi wa kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo-Cardiograph) wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kushirikiana na JKCI na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa wataalam wa afya kutoka hospitali mbalimbali nchini.
Wataalam wa afya kutoka hospitali mbalimbali nchini wanaoshiriki mafunzo ya kuchunguza jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo-Cardiograph) wakifuatilia mada iliyokuwa ikitolewa wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Mhadhiri mwandamizi na Dakatri bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Pilly Chillo akizungumza na washiriki wa mafunzo ya mwezi mmoja ya kufanya uchunguzi wa jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo-Cardiograph) wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na (MUHAS) kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa wataalam wa afya kutoka hospitali mbalimbali nchini.
Picha na: JKCI
…………………….
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
14/04/2022 Madaktari, Radiografa na Mafundi sanifu wa moyo (Cardiovascula Technologist) 29 kutoka hospitali mbalimbali nchini washiriki mafunzo ya wiki nne ya kufanya uchunguzi wa jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo-Cardiograph) yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (NMH).
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo uliofanyika jana katika Ukumbi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) Dkt. Pilly Chillo amesema kuwa mafunzo hayo ni ya awamu ya pili kufanyika baada ya yale yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mwezi Oktoba maka 2021.
Chillo ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo amesema ilikua ni ndoto yake kupeleka taaluma ya uchunguzi wa jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo-Cardiograph) kwa wataalam wengi wa afya kutokana na ongezeko kubwa la magonjwa ya moyo hapa nchini.
“Hapa JKCI ambako kuna wataalam wabobezi wa magonjwa ya moyo wanajua kufanya uchunguzi wa jinsi moyo unavyofanya kazi lakini wagonjwa wengi wapo mikoani na wataalam walioko huko hawana mafunzo maalum hivyo tukaona ni vyema kutoa mafunzo haya mara kwa mara ili kuwawezesha wataalam wa afya walioko mikoani kuwabaini na kuwapatia huduma stahiki wagonjwa wa moyo kwa wakati”,
“Uhitaji wa mafunzo haya ni mkubwa na lengo letu ni kuwafikia wote wanaohitaji mafunzo haya, awamu hii ya pili imewahusisha wataalam wa afya 29 kutoka mikoa mbalimbali nchini, awamu ya kwanza ya mafunzo haya ilikuwa na washiriki 41 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini pamoja na washiriki kutoka nchi za Somalia na Rwanda”, alisema Dkt. Chillo
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi amesema kuwa mafunzo hayo yaliyowahusisha wataalam wa afya kutoka hospitali binafsi na hospitali za serikali nchini hufanyika kwa nadharia kwa muda wa wiki mbili na wiki mbili zingine wataalam hao hufanya mafunzo kwa vitendo.
Prof. Janabi amesema kuwa ushirikirikiano uliopo baina ya JKCI, MUHAS na MNH ni moja ya tija kwa wakufunzi hao kwani watakaporejea katika sehemu zao za kazi na kuanza kufanya kwa vitendo yale waliyojifunza ni rahisi kwao watakapokutana na kesi ngumu kutuma picha na video walizowafanyia wagonjwa uchunguzi wa jinsi moyo unavyofanya kazi katika taasisi hizo tatu nao kwa pamoja watashirikiana kutatua kesi hizo.
“Wakufunzi hawa watakuwepo hapa JKCI kwa ajili ya kujifundisha yale ya msingi katika kutambua matatizo ya moyo hivyo kupunguza rufaa ambazo zingeweza kutatuliwa huko kwa kutambua ugonjwa na kufanya rufaa haraka pale wanapokutana na tatizo kubwa”,
“Naamini wakufunzi hawa wametoka kwenye hospitali ambazo wana mashine ya kutambua jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo-Cardiograph) hivyo nitawakie mafunzo mema, wakasome kwa bidii ili waende kuwa na tija katika hospitali wanazotoka na kuwa sehemu ya kuokoa maisha ya wagonjwa wanaowategemea”,
“Haya ni mafunzo muhimu na endelevu, rai yangu kwa hospitali zote nchini ni kutumia fursa hii kuwapa nafasi madaktari kujifunza, kuona na kufanya kwa vitendo uchunguzi wa jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo-Cardiograph)”, alisema Prof. Janabi
Naye mkufunzi kutoka hospitali ya Manispaa ya Kigoma Ujiji Dkt. Kalegamya Hinyuye amesema kuwa ni muda muafaka kwake kushiriki mafunzo ya kufanya uchunguzi wa jinsi moyo unavyofanya kazi (Echo-Cardiograph) kwani kumekuwa na uhaba mkubwa wa vifaa na wataalam wabobezi wa magonjwa ya moyo katika hospitali za mikoani hivyo kuwatibu wagonjwa hao kwa upofu (Blindly).
“Tumekuwa tukikutana na watoto ambao wana dalili zote za ugonjwa wa moyo lakini kutokana na changamoto ya utaalam wa kufanya uchunguzi wa jinsi moyo unavyofanya kazi tunashindwa kuthibitisha kuwa mtoto ana tatizo hilo hivyo kushinda kufanya maamuzi sahihi”,
“Mafunzo haya yamekuwa na tija kubwa kwangu, walimu wetu wametufundisha kuwa matibabu ya moyo hasa ya watoto yanapaswa kufanyika kwa wakati mfano kuna baadhi ya upasuaji wa moyo kwa watoto unapaswa kufanyika mtoto anapokuwa na umri wa wiki tatu baada ya kuzaliwa. Naamini watoto wengi wamekuwa wakipoteza maisha ndani ya kipindi hicho kutokana na uhafifu wa utaalam wa kuwagundua jinsi moyo unavyofanya kazi kwa wagonjwa”,
“Nikirudi katika sehemu yangu ya kazi nitakuwa balozi mzuri kwa kuwaona wagonjwa wanaopatikana katika mkoa wangu, wanaohitaji kupatiwa huduma huko nitahakikisha wanapatiwa kwa wakati na wale wanaohitaji rufaa ya kufika JKCI nao nitahakikisha wanapatiwa rufaa ili waweze kupata huduma hizi muhimu kwa wakati na kurejesha afya zao”, alisema Dkt. Hinyuye.