Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akifungua kikao kazi cha ofisi yake na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi jijini Dodoma kilichoandaliwa kwa lengo la kupata maoni ya wadau yatakayoboresha mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa watumishi wa Umma (Public Employees Performance Management Information System-PEPMIS) ambao utaanza kutumika rasmi kuanzia mwezi Julai, 2022.
Baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) wakati akifungua kikao kazi cha ofisi yake na viongozi hao, kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kupata maoni ya kuboresha mfumo mpya wa usimamizi wa utendaji kazi kwa Watumishi wa Umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira, Vijana na Wenye, Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi wakifuatilia mada kuhusu mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa watumishi wa Umma utakaoanza kutumika rasmi Serikalini kuanzia mwezi Julai, 2022.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira, Vijana na Wenye, Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akifunga kikao kazi Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi jijini Dodoma, kilichoandaliwa kwa lengo la kupata maoni ya wadau yatakayoboresha mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa watumishi wa Umma utakaoanza kutumika rasmi Serikalini kuanzia mwezi Julai, 2022.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira, Vijana na Wenye, Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Vyombo vya Habari kuhusu umuhimu wa kikao kazi za Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kilichofanyika jijini Dodoma.
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamhokya akizungumza na Vyombo vya Habari kuhusu ushiriki wa Vyama vya Wafanyakazi kwenye kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Bw. Deus Seif akizungumza na Vyombo vya Habari kuhusu ushiriki wa CWT kwenye kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora jijini Dodoma.
………………………..
Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, ofisi yake imevishirikisha Vyama vya Wafanyakazi ili kupata maoni na ushauri utakaoisaidia Serikali kupata mfumo mpya mzuri wa kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma utakaochukua nafasi ya mfumo wa awali wa OPRAS ambao umebainika kuwa na mapungufu wakati wa kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma.
Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha ofisi yake na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kilichoandaliwa kwa lengo la kupata maoni ya wadau yatakayoboresha mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa watumishi wa Umma (Public Employees Performance Management Information System-PEPMIS) ambao utaanza kutumika rasmi kuanzia mwezi Julai, 2022.
Mhe. Jenista amesema, wakati ofisi yake iko katika hatua za mwisho kukamilisha mfumo huo mpya wa kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma, aliona kuna ulazima wa wadau kupitishwa kwenye mfumo huo na ndio maana alielekeza watendaji wa ofisi yake kuandaa kikao kazi na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi ili kupata maoni ya kuuboresha.
“Tushaurini vizuri ili tupate mfumo bora wa kupima utendaji kazi wa watumishi ambao utaliwezesha taifa kuwa na Watumishi wa Umma wanaowajibika bila kushurutishwa kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista amesema, dhamira yake ya muda mrefu ni kutamani kuona Watumishi wa Umma wanafanya kazi muda wote wa kazi na ikitokea mtumishi anakosa kwenda kazini kwa sababu yoyote ile ahuzunike kwa kitendo hicho.
Ameongeza kuwa, Serikali inatamani mfumo huo mpya uwe na uwazi wa kutosha katika usimamizi wa Watumishi wa Umma, uwe ni mfumo ambao utaondoa kabisa upendeleo, uonevu na upime utendaji kazi wa watumishi kwa haki ili kuendana na dhamira ya Mhe. Rais ya kuujenga Utumishi wa umma unaowajibika kwa hiari.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira, Vijana na Wenye, Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, amesema kikao kazi hicho kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais-UTUMISHI ni kikao muhimu sana kilichotoa fursa kwa Vyama vya Wafanyakazi kushiriki kikamilifu katika kutoa mchango wa kuboresha mfumo ambao utawawezesha Watumishi wa Umma kuendelea kuwajibika ipasavyo.
Mhe. Ndalichako ameongeza kuwa, maoni ya Viongozi hao wa Vyama vya Wafanyakazi yatasaidia utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais ya kuwataka Watumishi wa Umma kufanya kazi na kuwajibika kwa hiari.
Akizungumzia mwaliko wa kushiriki kikao kazi hicho, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Bw. Tumaini Nyamhokya ameshukuru kwa mwaliko wa kushiriki kikao kazi hicho ambacho kimewapa fursa ya kutoa maoni na ushauri utakaoboresha mfumo mpya wa kusimamia na kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma nchini.
Naye, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Bw. Deus Seif amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kitendo cha ofisi yake kusanifu mifumo ya usimamizi wa utendaji kazi wa Watumishi wa Umma nchini ambayo ni rafiki kuitumia.
Kikao kazi hicho cha siku moja kilichofunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na kufungwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, kimehudhuriwa na Vongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kutoka TUCTA, TUICO, RAAWU, TUGHE, TEWUTA, TPAMU, TAMCO, COTWU (T), DOWUTA, CHODAWU, CWT, TALGWU, TRAWU na TASU.