Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akimkabidhi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald Wright (kushoto) katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba, jijini Dar es Salaam. (Picha na Adam H. Mzee/CCM Makao Makuu)
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Ndugu Daniel Chongolo akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar wakipokutana Ofisi Ndogo ya Makao Makuu Lumumba jijini Dar es Salaam Leo.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM akizungumza na Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania, Regine Hess,
…………………………………..
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo kwa nyakati tofauti amekutana na Kufanya Mazungumzo na Balozi wa Marekani, Ujerumani na Uingereza.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo Ijumaa tarehe 08 Aprili, 2022 katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu Lumumba jijini Dar es salaam.
Awali, Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald Wright akizungumza na Katibu Mkuu pamoja na mambo mengine, ameeleza utayari wa Marekani kuendeleza ushirikiano uliopo katika maeneo mbalimbali hasa Sekta ya Afya, Biashara na uwezeshaji wa Vijana na wanawake kiuchumi.
Katibu Mkuu, katika mazungumzo hayo, ameeleza kwa undani namna Serikali ya CCM inavyoshughulika katika nyanja mbalimbali za kuboresha maisha ya wananchi, ikwemo katik sekta ya Elimu, Afya na uwezeshaji wa Wanawake na Vijana kiuchumi hivyo ushirikiano kati ya Mataifa haya mawili utaendelea kukuza zaidi jitihada za kuongeza ustawi wa wananchi wa Tanzania.
Aidha, Balozi wa Ujerumani Nchini Tanzania, Regine Hess, amesifu uhusiano mzuri wa kihistoria unaoendelea kudumishwa baina ya Tanzania na Ujerumani, ambapo, ameeleza kuridhishwa na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na yeye ataendelea kuwashawishi wawekezaji kutoka Ujerumani kuja kuwekeza mitaji nchini Tanzania ili kukuza ustawi wa wananchi.
Katibu Mkuu akieleza mazingira rafiki ya uwekezaji nchini, amemuhakikishia Balozi Hess kuwa, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuhimiza Serikali zake zote mbili ili kuendelea kuweka mazingira rafiki zaidi ya uwekezaji na yenye tija kwa pande zote yaani Tanzania na Wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar pamoja na mambo mengine, ameeleza utayari wa Uingereza katika kuendelea kukuza ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwezo Biashara, Kilimo na Utunzaji wa Mazingira.
katibu Mkuu, akizungumza na Balozi huyo, ameeleza umuhimu wa ushirikiano hasa katika uhifadhi wa mazingira ikiwemo kuelimisha wafugaji katika kutunzaji mazingira, ambapo amesisitiza kuwa bila Wafugaji kupewa elimu za uhifadhi wa mazingira hata kilimo kitakuwa katika mazingira magumu kuendelea.
Kwa ujumla, Mabalozi hao wameeleza kufurahishwa na utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali hasa katika kuendelea kukuza mazingira rafiki ya uwekazaji nchini.