Mratibu wa Mradi wa Shirika la Jiokoe na Umaskini yaani Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) Benard Maira, akiupiga mwingi wakati akizungumza kwenye kikao hicho. |
Afisa wa Polisi Dalahile Mahende wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Ikungi, akizungumzia namna wanavyozipokea kesi hizo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Siuyu, John Ghumpi akichangia jambo kwenye kikao hicho. |
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Unyankanya, Nicomedy Senge akichangia jambo kwenye kikao hicho |
Picha ya mshikamano baada ya kikao hicho.
|
Na Dotto Mwaibale, Singida SHIRIKA la Jiokoe na Umaskini yaani Stars of Poverty Rescue Foundation (SPRF) kupitia mradi wa ‘AWARE 2020’ limeibua ukatili mkubwa wa kijinsia wa Baba mmoja mkazi wa Kijiji cha Damankia katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida (jina lake tunalihifadhi) ambaye hajishughulishi kuhudumia familia yake kudaiwa kukojolea unga na mboga kwa lengo la kumkomoa mke wake na watoto baada ya kudaiwa kulewa na kutishiwa kutopewa chakula.
Imeelezwa kwamba licha ya tukio hilo lililotokea Septemba 9 mwaka jana na kufikishwa ngazi ya kata hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo ambaye inaelezwa amekuwa akirudia mara kwa mara kufanya vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya familia yake.
Tukio hilo liliibuliwa na Katibu wa Kamati za Vijiji za Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) wa kijiji hicho Mwalimu Salima Hassan Hole wakati akitoa taarifa kwenye kikao cha Watekelezaji wa Sheria kilichoketi kwa ajili ya kuhimiza utekelezaji wa mkakati wa kushughulikia kesi za ukatili wa kijinsia kilichofanyika hivi karibuni wilayani humo.
Wadau waliokutanishwa na shirika hilo katika kikao hicho ni makatibu wa kamati za MTAKUWWA wa kata hizo, Jeshi la Polisi, Wenyeviti wa vijiji, maafisa watendaji wa vijiji, mahakama, Madiwani wa kata ulipo mradi huo, lengo likiwa ni kushughulikia kesi zinazowahusu watuhumiwa wa vitendo vya ukatili (kama ubakaji, ulawiti, ukeketaji, ndoa za utotoni) , vipigo kwa wanawake na ukatili kwa watoto katika vijiji vinne vya mradi ndani ya wilaya hiyo ambavyo ni Siuyu na Unyankhanya vilivyopo Kata ya Siuyu, Munkinya na Damankia kutoka Kata ya Dung’unyi.
Kikao hicho cha wadau kilifanya majadiliano yaliyolenga kupata ufumbuzi na mbinu bora za kushughulikia kesi mbalimbali za vitendo vya ukatili wa kijinsia ambazo nyingi zimekuwa zikiwanyima haki waathirika kutokana na sababu mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa SPRF nchini, Dkt.Suleiman Muttani alisema shirika hilo chini ya ufadhili wa Foundation for Civil Society (FCS) limekuwa likitekeleza mradi wa AWARE katika kata nne za Wilaya ya Ikungi kwa kufanya utetezi wa haki za wanawake na mtoto wa kike dhidi ya athari zitokanazo na mila na desturi kandamizi lakini kesi nyingi zimekuwa zikiishia njiani kutokana na sababu mbalimbali ndio maana wakaitisha kikao hicho cha watekelezaji wa sheria ili kupata majibu na kuona ni njia gani itakayosaidia kuzisukuma mbele ili wahanga wapate haki zao.
Muttani alisema kuwa baada ya mradi huo wanatarajia kuanzisha vituo vya taarifa na maarifa ambavyo vitakuwa vikipokea taarifa za matukio ya ukatili kutoka makundi mbalimbali na kuwa zitakuwa zikipokelewa na watu makini huku wakihusishwa viongozi wa dini, mila na watu maarufu na baada ya hapo yatafanyika majumuisho ili kujua changamoto zilizokuwepo wakati wa kuzikusanya na mafanikio waliyopata.
Katika kikao hicho mambo mengi yaliibuka yakiwemo ya kuonekana kwa matukio mengi ya ukatili yakifanyika katika jamii huku yanayofikishwa polisi yakiwa machache na kesi zake zikishindwa kupata ushindi kutokana na kukosa ushahidi baada ya watuhumiwa na ndugu za waathirika kukaa na kuyamaliza kienyeji bila ya kufuata mkondo wa sheria.
Afisa wa Polisi Dalahile Mahende wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Ikungi alisema katika kipindi cha kutoka Oktoba mwaka jana hadi Machi mwaka huu makosa ya ukatili wa kijinsia waliyopokea kutoka vijiji vinne vya mradi yalikuwa 21 kati ya makosa hayo lugha za matusi yalikuwa mawili ambayo yalipelekwamahakama.
Alisema kesi moja ilipata ushindi na nyingine bado inaendelea kusikilizwa na kuwa kesi ya pili ilikuwa ni ya shambulio ambayo ilikuwa na makosa 13 lakini yaliyofanyiwa kazi yalikuwa ni yale yaliohusu ukatili wa kijinsia kati ya mke, mume na watoto na mahakamani yalienda matano na yaliyopata mafanikio ni mawili, moja inaendelea na hizo zingine zilisuluwisha na polisi.
Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Ikungi, Mrakibu wa Polisi (SP) Stephen Chaula alisema matukio yote ya ukatili wa kijinsia ambayo ni makubwa lazima yafikishwe kituoni hapo yakitokea kwenye vituo vyao vidogo saba vilivyopo katika kata mbalimbali na yale madogo wanayajadili na wakiona yana mashiko wanayapeleka mahakamani.
Chaula alisema sio kila tukio linalotokea ni lazima yafanyike majadiliano akitolea mfano tukio la kubaka au kumpa mimba mwanafunzi matukio hayo ni kukamilisha upelelezi na kuwapeleka wahusika mahakamani.
“Kwa matukio hayo hatuna mjadala na mtuhumiwa kama kumpa mimba mwanafunzi au kubaka na pengine anakuwa na magonjwa ya kuambukiza hapo hatuna msamaha” alisema Chaula.
Chaula alisema hata wazazi watakao bainika wamemuoza mtoto wao kwa mwanaume kutokana na tamaa ya fedha licha ya kujua ni mwanafunzi hawatakuwa salama ni lazima watawakamata pamoja na muoaji na kuwafikisha kwenye mkono wa sheria.
Katika kikao hicho Makatibu wa Kamati za MTAKUWWA kutoka kata za mradi walitoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia na kuelezea namna walivyo yashughulikia ikiwa ni pamoja na kuyafikisha ngazi tofauti kwa hatua nyingine zaidi.