Na Hellen Mtereko, Mwanza
Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko iliyopo chini ya Wizara ya Kilimo Kanda ya Ziwa imejikita kuzalisha mchele,unga wa sembe kwenye kiwanda chao ambacho kimeanza kufanya kazi hivi karibuni Jijini Mwanza.
Hayo yamebainishwa leo hii Aprili 5,2022 na Meneja wa bodi hiyo Kubena Stephen, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya ongezeko la bei katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani.
Amesema katika kipindi hiki cha mfungo wafanyabiashara wengi hupandisha bei za vyakula, ndio maana wanauza maharage,korosho,dengu,ufuta pamoja na mazao mengine wanayoyanunua kutoka kwa wakulima ili Jamii iweze kununua kwa bei nafuu.
“Tumekuwa na utaratibu wa kununua mpunga kutoka kwa wakulima moja kwa moja bila kupitia kwa madalali lengo kubwa ni kuwainua kiuchumi,tukisha ununua tunaukoboa wenyewe ukiwa na ubora wa hali ya juu na ukiwa tayari tunawauzia Wananchi kwa bei nafuu”,amesema Steven.
Amesema mazao wanayoyakoboa wanauza kwenye mahotel mbalimbali,mwananchi mmoja mmoja pamoja na jumla lengo ikiwa ni kupunguza mzigo wa bei kubwa kwa Wananchi waliopo kanda ya ziwa na maeneo mbalimbali nchini.
Stephen amesema kuwa wamekuwa wakiwajali na kuwathamini wakulima wadogo wa mpunga na mahindi kwani kila mkulima anayefikisha mzigo wake kwao analipwa fedha siku hiyo hiyo.