Meneja wa ubia, uwezeshaji na mawasiliano kwenye mradi mtambuka wa saratani (TCCP) kutoka Hospital ya Aghakan Dk.Sarah Maongezi akizungumza na waandishi wa habari leo hii Jijini Mwanza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya kuielimisha jamii namna ya kujiepusha na magonjwa ya saratani
Dakitari Beda likonda bingwa wa magonjwa ya saratani aliyebobea kwenye tiba ya mionzi kutoka Hospital ya kanda ya Bugando iliyoko Jijini Mwanza akizungumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Taasisi ya Aghakan
…………………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Taasisi ya Aghakan kupitia mradi mtambuka wa saratani (TCCP) unaofadhiliwa na shirika la maendeleo la Ufaransa (AFD) imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari 37 Jijini Mwanza.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya kuielimisha jamii namna ya kujiepusha na magonjwa ya saratani.
Mradi huo wenye thamani ya Euro 13.3m unatekelezwa katika wilaya 13 za Mikoa ya Mwanza na Dar es salaam na unatarajia kukamilika mwaka 2024.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo Meneja wa ubia,uwezeshaji na mawasiliano kwenye mradi mtambuka wa saratani kutoka Taasisi ya Aghakan, Dk.Sarah Maongezi amesema kuwa jamii bado inauelewa mdogo juu ya ugonjwa wa saratani hivyo kupitia mafunzo hayo waandishi watakuwa chachu ya kuwaelimisha namna ya kuepukana na ugonjwa huo.
Amesema mradi huo unatarajia kununua gari la uchunguzi wa saratani ambalo litakuwa na mashine ya uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti na litasaidia kusogeza huduma karibu kwa Wananchi haswa kwa wale ambao wapo Vijijini.
Kwa upande wake Dakitari bingwa wa magonjwa ya saratani aliyebobea kwenye tiba ya mionzi kutoka Hospital ya kanda ya Bugando, Beda Likonda amesema kuwa kwa mwaka Tanzania inapata wagonjwa wapya elfu 40000 wenye matatizo ya saratani kati ya hao asilimia 25 ni wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.
Naye Dakitari bingwa wa upasuaji kutoka Hosptali ya Rufaa ya Mkoa Sokouture Dk.Athanas Ngambakubi amesema kuwa utumiaji wa tumbaku na pombe kupita kiasi huchangia kwa kiasi kikubwa katika maambukizi ya magonjwa ya saratani.
Amesema dalili za awali za ugonjwa wa saratani ni kutokwa na damu sehemu za siri kwa wanawake tofauti na hedhi,uvimbe kwenye matiti, uvimbe kwenye kwapa,kupungua kwa uzito,maumivu makali ya kiuno,nyonga na mgongo.
Amesema kuwa jamii iwe na utatatibu wa kufika kwenye vituo vya afya kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya zao pindi waonapo dalili hizo ili watakapo baini tatizo wataalamu waweze kuwasaidia kabla ya ugonjwa huo kusambaa.