Kaimu Kamishina wa ardhi akizungumza na waandishi wa habari
********************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wadaiwa sugu 400 wa kodi ya ardhi Mkoa wa Mwanza wamefikishwa Mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Machi 18, 2022 kabla ya kesi kuanza, Kaimu Kamishina wa ardhi Mkoa wa Mwanza, Elia Kamihanda amesema kuwa wadaiwa hao kutoka Wilaya za Nyamagana na Ilemela wanadaiwa zaidi ya bilioni 4.
“Ofisi ya ardhi Mkoa wa Mwanza leo tumeanza rasmi kuchukua hatua za kisheria za kuwafikisha wamiliki wa ardhi wote ambao wamevunja sharti la umiliki la kulipa Kodi ya ardhi kwa wakati,na kwa mujibu wa sheria”,amesema Kamihanda.
Amesema wanatarajia awamu ya pili kuanza na Halimashauri ya Magu kwani wamesha sambaza ilani yenye deni la milioni 700 na wao wasipo lipa watawafikisha mahakamani.
Amesema kwa kuzingatia takwa la sheria inayoongozwa na kifungu namba 50 cha sheria ya ardhi mmliki wa ardhi endapo atashindwa kulipa kodi kwa wakati atafikishwa mahakamani ili iweze kuwasaidia katika kukusanya mapato ya Serikali.
Kamihanda amesema kuwa kwa mwaka jana walikusanya kodi ya ardhi sh. bilioni 8 ambapo kwa mwaka huu wamelenga kukusanya maduhuli ya Serikali yatokanayo na huduma ya Sekta ya ardhi sh. bilioni 18.
Ameeleza kuwa changamoto kubwa ambayo inaikumba Ofisi ya ardhi Mkoani Mwanza ni baadhi ya wamiliki kutokuwa na utayari wa kulipa kodi ya ardhi hivyo kuchelewesha upatikanaji wa mapato.
Mwisho Kamihanda ametoa wito kwa wamiliki wa ardhi kuwa na utatatibu wa kulipa kodi zao kwa wakati ili kuondokana na changamoto ya kufikishwa Mahakamani.