Makamu wa Kwanza wa Rais Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akihutubia na kufungua rasmi mafunzo ya siku ya tatu kwa wafanyakazi wa kitengo cha Tiba ya mgongo na mishipa ya fahamu ,yanayohusu tiba ya uvimbe na saratani ya ubongo huko Hospitali ya Rufaa Mnazi mmoja Zanzibar.
Mfanyakazi kitengo cha Tiba ya mgongo na mishipa ya fahamu (NED) dkt.Mulhat Simba akisoma risala kwa niaba ya kitengo hicho wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya tiba ya uvimbe na saratani ya ubongo yaliyofanyika Hospitali ya Rufaa Mnazi mmoja Zanzibar.
Waziri wa Afya Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akizungumza machache na kimkaribisha mgeni rasmi Makamu wa Kwanza wa Rais Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman kuhutubia na kufungua mafunzo ya tiba ya uvimbe na saratani ya ubongo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hyssein Ali Hassan Mwinyi huko Hospitali ya Rufaa Mnazi mmoja Zanzibar.
***********************************
Na Sabiha Khamis Maelezo 18/03/2022
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Othman Masoud Othman ameitaka Taasisi ya Tiba ya mgongo na mishipa ya fahamu katika hospital ya Mnazi Mmoja kuendelea na utaratibu wa kutoa mafunzo ya kitaalamu kwa watendeji wa kitengo hicho ili kuongeza elimu, ufanisi na weledi kwa watendaji wake.
Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matibabu ya uvimbe na saratani ya ubongo yaliyofanyika Hospital ya Mnazi Mmoja.
Amesema kuwepo na tabia ya kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watendaji ni jambo muhimu kwani huwaongezea uwezo wafanyakazi katika kukamilisha majukumu yao ya kazi za kila siku
Amesema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza gharama kwa Serikali katika kuwalipia wagonjwa wanaohitaji kusafirishwa na kupatiwa tiba nje ya nchi na badala yake kutibiwa ndani ya nchi kwa kupata huduma bora na kwa idadi stahiki.
Aidha amewataka wataalamu hao kuzidisha bidii, juhudi na kuyapa umuhimu mafunzo hayo ili kuleta matokeo yenye tija kwa hospital na jamii kwa ujumla.
Vile vile ameipongeza Taasisi hiyo kwa ushirikiano wa karibu na Daktari bingwa kutoka Spain kwa kufanikisha mafunzo haya yenye lengo la kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya katika Nyanja mbali mbali.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui amesema Taasisi hiyo inatambulika Afrika Mashariki katika utendaji wake wa kazi hivyo ni vyema kuyafanyia kazi mafunzo watakayopewa ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Amesema kuna wagonjwa wengi kutoka Pemba hivyo mipango ya Serikali ni kuanzisha Taasisi hicho kisiwani humo ambapo hadi sasa imekamilisha baadhi ya vitengo ikiwemo CT Scan na ICU Unite.
Nae rais wa taasisi ya tiba ya mgongo na mishipa ya Fahamu NED Foundation Prof. Jose Piquer amesema atashirikiana na Serikali ili kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu ili kuwapatia ujuzi zaidi madaktari.
Jumla ya kesi 1850 zimefanyiwa upasuaji ikiwemo uvimbe wa kichwa, ajali za kichwa na mgongo, watoto wenye vichwa maji na mgonga wazi tangu kuazishwa kwa kitengo hicho mwaka 2014.