Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mamlaka ya Kudhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA) imetoa mafunzo ya sheria ya ununuzi wa Umma kwa wajumbe wa Bodi za zabuni Jijini Mwanza.
Mafunzo hayo ya siku 4 yamehudhuriwa na washiriki 100 kutoka taasisi mbalimbali wakiwemo wajumbe wa Bodi za zabuni,wakuu wa vitengo vya ununuzi pamoja na wanasheria.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo kaimu Mkurugenzi wa idara ya kujenga uwezo na huduma za ushauri kutoka PPRA, Castor Komba amesema kuwa wanatoa mafunzo hayo ili kuwajengea uelewa wa sheria na taratibu za manunuzi ya Umma kwenye taasisi zao.
Amesema kuwa Mamlaka ya Kudhibiti Manunuzi ya Umma (PPRA) inawajibu wa kuhakikisha Taasisi nunuzi wanatekeleza majuku yao katika ununuzi wa Umma kwa kuzingatia sheria na taratibu.
Amesema kuwa wamekuwa wakitoa miongozo mbalimbali na hivi karibuni wametoa muongozo wa Uviko-19 ambao ulitokana baada ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kupokea msaada wa zaidi ya Trilioni 1.3.
” Tulitoa muongozo wa namna gani fedha hizo zinaweza kutumika na kuleta thamani katika manunuzi ya Umma na ndio maana kwa sasa miradi mingi inatekelezwa kwa kuzingatia muongozo wa Uviko-19″, amesema Komba.
Ameleeza kuwa kwa sasa wanafanya ukaguzi wa miradi inayoendelea kutekelezwa kwa fedha za Uviko-19 ambapo kwa taarifa za wakaguzi miradi hiyo imefanyika kwa kuzingatia sheria
Dr. Alex Kimambo mjumbe wa Bodi ya manunuzi kutoka Hospital ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma ni miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo, amesema pamoja na kwamba siyo mtaalamu wa sheria,fursa hiyo imempa uwezo wa kutambua umuhimu wa kufanya manunuzi yenye tija kwa kuzingatia sheria hali itakayosaidia fedha zonazotolewa na Serikali kutumika ipasavyo.