Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, akimsikiliza Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Philemoni Bagambilana, wakati Naibu Waziri huyo alipozungumza na Menejimenti ya Kampuni hiyo, jijini Mwanza.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, akimsikiliza Meneja Mradi wa Meli ya MV Mwanza, Luteni Kanali Mhandisi Vitus Mapunda (kulia) wakati akimweleza maendeleo ya Ujenzi wa Meli hiyo, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea mradi huo jijini Mwanza.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, akitoa maelekezo kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Philemoni Bagambilana (wa pili kulia), wakati Naibu Waziri huyo alipokagua mradi wa meli ya MV Mwanza, jijini Mwanza.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, akikagua maeneo mbalimbali ya meli ya MV. Umoja inayofanyikwa ukarabati katika bandari za Mwanza jijini Mwanza.
Meneja Mradi wa wa MV. Umoja, Mhandisi Elias Kivara akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Uchukuzi), Atupele Mwakibete, kuhusu hatua iliyofikiwa ya ukarabati wa meli hiyo wakati wakati Naibu Waziri huyo maendeleo ya ukarabati wake, jijini Mwanza.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa meli ya MV Mwanza inayojengwa jjijini Mwanza ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu.
PICHA NA WUU
…………………….
Imeelezwa kuwa kukamilika kwa ujenzi wa meli ya MV Mwanza na Ukarabati wa meli ya MV Umoja kutarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kwa mikoa inayozunguka Mkoa wa Mwanza pamoja na nchi Jirani zinazotumia Ziwa Victoria.
Kauli hiyo imetolewa jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete mara baada ya kukagua maendeleo ya ukarabati na ujenzi wa meli hizo kusema Serikali itaendelea kutenga fedha ili kukamilisha miradi yote ya Kampuni ya Huduma za Meli.
“Nipende kuwahakikishia kuwa kukamilika kwa ujenzi wa meli ya MV Mwanza kutatochea sana uchumi na kuongeza pato kwa mikoa inayozunguka Ziwa lakini pia kukamilika kwa ukarabati wa MV Umoja kutarahisisha sana usafiri wa abiria na mizigo”, amefafanua Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete ameitaka Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kuhakikisha inawasimamia kwa karibu Wakandarasi wote wawili wanaotekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati ili wakamilishe miradi hiyo kwa kuzingatia thamani ya fedha lakini kuongeza ujuzi kwa wataalaam wa ndani.
Aidha, Naibu Waziri Mwakibete ameihakikishia MSCL kuwa changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo upungufu wa watumishi wa fani za uhandisi kuwa litashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi ili kufanya taasisi hiyo iweze kuwa imara kiutendaji.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa MSCL, Philemoni Bagambilana, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa taasisi imejipanga na inasimamia kwa karibu miradi hiyo ili kuleta matokeo ya uwekezaji unaofanywa na Serikali katika ukanda huo.
Bagambilana ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza kwenye taasisi hiyo na kusema moja ya matokeo ya uwekezaji kwenye ukarabati wa meli hasa za MV Victoria na MV Butiama ni kuongezeka kwa mapato kutoka bilioni takribani 1 kwa mwaka 2019 hadi kufikia bilioni takribani 4.5 mwaka 2021.
Mradi wa Ujenzi wa Meli ya MV Mwanza unatekelezwa na Kampuni ya Gas Entec Company Limited na Kampuni ya KANGNAM Corporation kwa kushirikiana na SUMA JKT kwa gharama ya shilingi bilioni 96.9 na ukarabati wa Meli ya MV Umoja unatekelezwa na SM Solution Co ltd ya nchini Korea na unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 19.
(Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi)