Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Khadija Shaban-Keisha- (kushoto) akisalimiana leo mjini Tanga na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) wakati Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria walipowasili Mkoani Tanga kwa ajili ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya Mahakama.
aibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Pinda ( kushoto kutoka mlango wa basi) akisalimiana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel(kulia) leo mjini Tanga wakati alipoongozana na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa ajili ya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya Mahakama.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Pinda (katikati) leo mjini Tanga wakati alipoongozana na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa ajili ya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya Mahakama.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akitoa maelezo mafupi leo Mjini Tanga ya kuwakaribisha Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa ajili ya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ya Mahakama.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Pinda (kushoto) akitoa salamu za Serikali kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria leo walipotembelea kukagua mradi wa jengo la kuhifadhia nyaraka la Mahakama Kuu kanda ya Tanga.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akitoa shukurani kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria leo mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Tanga la kuhifadhia nyaraka.
Picha na Mahakama ya Tanzania
……………………………………..
Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania
Ujenzi wa Jengo la Mahakama ya wilaya ya Mkinga, Mkoani Tanga ambalo litagharimu shilingi bilioni 1.1 hadi kukamilika utamalizika mwishoni mwa Mwezi wa Aprili mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa leo Mjini Tanga na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel wakatiakitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ambayo iko katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya Mahakama.
Alisema kukamilika kwa Jengo hilo utakuwa faraja kwa wananchi wa Wilaya ya Mkinga na kuuwezesha Mkoa wa Tabora kuwa na Mahakama kila Wilaya.
Prof. Gabriel aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inaoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha Mahakama ya Tanzania fedha za kuboresha miundombinu kwa ajili ya kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Tunamshukuru Mama yetu Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuitazama Mahakama ya Tanzania kwa jicho la pekee ambapo anaendelea kutuwezesha fedha za kujenga majengo mbalimbali ikiwemo Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania mjini Dodoma ambayo itamalizika Desemba mwaka huu na itagharimu bilioni 129.7”aliongeza.
Prof. Gabriel alisema kukamilika kwa majengo hayo mjini Dodoma yatafanya Mahakama ya Tanzania kuwa na majengo mazuri na ya kisasa kwa upande wa Afrika Mashariki na kwa Nchi za SADC.
Aidha Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama ya Tanzania alisema Serikali ya Awamu ya Sita iko katika hatua za mwisho ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji haki 9 hadi 12 katika kanda mbalimbali hapa nchini.
Alisema mpango huo ukikamilika wa kujenga Vituo 12 utafikisha 18 na kuwezesha kila Kanda kuwa na Kituo kimoja baada ya vile Sita ambavyo vimeshajengwa.
Prof. Gabriel aliongeza kuwa wanatarajia kujenga Mahakama za Mwanzo 60 kwa ajili ya kusogeza huduma hiyo katika maeneo ambayo hayajafikiwa.
Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Geophrey Pinda alisema Serikali itahakikisha ifikapo mwaka 2025 Wilaya zote ziwe na huduma ya Mahakama ya Wilaya ili kusogeza huduma za utoaji wa haki karibu na wananchi.