Mchungaji Jacob Mutashi kutoka Kanisa la Kiloleli Jijini Mwanza akizungumza na waandishi wa habari juu ya mafanikio yaliyotekelezwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wake.
……………………………………..
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kufuatia siku 365 za uongozi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu, Mchungaji Jacob Mutashi kutoka Kanisa la E.A.G.T lililopo Kiloleli Jijini Mwanza amezungumzia maendeleo ya Nchi katika nyanja mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumanne Machi 15,2022 Mutashi amesema kuwa mafanikio mengi yameonekana katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wake ikiwemo, kujenga uhusiano na mataifa mengine hali itakayosaidia uchumi wa Nchi kuzidi kuimarika.
Amesema kuwa masuala ya kisiasa yameonekana kuboreshwa zaidi kwa kuteua nafasi mbalimbali za uongozi bila kuangalia dini, kabila, jinsia.
” Hapendelei upande wowote katika kufanya teuzi kikubwa anachopenda yeye watu anaowateuwa wafanye kazi kwelikweli ili kuweza kuiishi kauli mbiu yake ya “Kazi iendelee”, pamoja na baadhi ya watu walikuwa na imani ndogo kwake kwakuwa ni Rais wa kwanza Mwanamke Kuongoza Nchi lakini kwa huu mwaka mmoja ameonyesha ujasiri mkubwa wa kuliongoza Taifa kwa amani na utulivu na kuifanya Tanzania kuendelea kuilinda tunu ya amani tuliyopewa na Mungu”,amesema Mutashi.
Ameongeza kuwa Rais Samia amekuwa akikutana na makundi mbalimbali katika Jamii ambayo ni Wazee, Viongozi wa dini,wanawake,Vijana, wafanyabishara sanjari na kutimiza,kutatua masuala kadhaa yaliyokuwa yakiwakabili.
Mwisho ametoa wito kwa viongozi wa dini kuwa waendelee kumuombea Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu ili azidi kutumikia Taifa akiwa na afya tele.