Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Profesa. Joyce Ndalichako, akiongea na madaktari wanao husika katika kuwafanyia wafanyakazi tathmini ya ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi, wakati alipokuwa akifungua mafunzo kwa madaktari kutoka katika hospitali za mikoa, wilaya na wadau wengine, tarehe 14 Machi, 2022 mjini Morogoro,
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Dkt. John Mduma akifafnua umuhimu wa kuwa na miongozo iliyoandaliwa kwa Madaktari wa kufanya Tathmini za Ulemavu kuwa imezingatia matakwa ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura 263 na Kanuni za Fidia kwa Wafanyakazi za mwaka 2016 na marekebisho yake.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Profesa. Joyce Ndalichako,akizindua muongozo wa madaktari kufanya tathmini ya ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi, wakati alipokuwa akifungua mafunzo kwa madaktari kutoka katika hospitali za mikoa, wilaya na wadau wengine, tarehe 14 Machi, 2022 mjini Morogoro
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Profesa. Joyce Ndalichako, akiwa katika picha ya pamoja na madaktari wanao husika katika kuwafanyia wafanyakazi tathmini ya ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi, mara baada ya kufungua mafunzo kwa madaktari kutoka katika hospitali za mikoa, wilaya na wadau wengine, tarehe 14 Machi, 2022 mjini Morogoro,
.,………………..
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Profesa. Joyce Ndalichako, amewataka madaktari watakao husika katika kuwafanyia wafanyakazi tathmini ya ulemavu uliotokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi, kufanya tathmini hiyo kwa usahihi ili wafanyakazi hao waliougua au uumia ama kufariki wapate fidia stahiki na kwa wakati.
Profesa Ndalichako ameyasema hayo leo Jumatatu, tarehe 14 Machi, 2022 mjini Morogoro, alipokuwa akifungua mafunzo kwa madaktari kutoka katika hospitali za mikoa, wilaya na wadau wengine wanaohusika na kufanya tathmini hiyo.
Amefafanua kuwa kwa kuwa mafunzo hayo yameambatana na uzinduzi wa miongozo ya tathmini za ulemavu hivyo madaktari hawanabudi kuifuata miongozo hiyo ili wafanyakazi waweze kupata mafao bora ya fidia kwa ajili ya kuwawezesha kumudu maisha yao.
“Kumekuwepo na changamoto ya ufanyaji wa tathmini, mfanyakazi akienda kwa madaktari tofauti na tathmini zinakuwa tofauti. Kwa hatua hii ya mafunzo na miongozo iliyoandaliwa na WCF itawezesha tathmini kufanyika kwa ufanisi. Hivyo nawaelekeza WCF muandae kanzidata ya waliopata mafunzo haya ili kuweza kupata mrejesho wa huduma zetu” amesisitiza Ndalichako.
Mhe. Ndalichako amefafanua kuwa uwepo wa WCF ni hatua muafaka katika mazingira ya sasa ambapo Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea na kazi ya kujenga uchumi wa viwanda na hivyo kuwa na ongezeko kubwa la maeneo ya uzalishaji linalokwenda sambamba na ongezeko la matukio ya ajali au magonjwa yatokanayo na kazi.
“Katika mazingira haya, jukumu la Mfuko siyo kulipa fidia pekee bali pia kushirikiana na wadau katika kubuni, kukuza na kuendeleza mbinu za kupunguza ama kuzuia kabisa ajali na magonjwa katika maeneo ya kazi. ”Amesema Ndalichako.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Dkt. John Mduma
ameeleza kuwa miongozo iliyoandaliwa imezingatia matakwa ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura 263 na Kanuni za Fidia kwa Wafanyakazi za mwaka 2016 na marekebisho yake.
“Miongozo hii itatumika katika mafunzo haya ili kuwajengeeni uwezo wa kufanya tathmini za ulemavu kwa usahihi. nikuhakikishie kuwa matumizi ya miongozo hii itaongeza ufanisi na urahisi katika kufanya tathmini za ulemavu na kuwezesha WCF kuchakata madai ya fidia kwa wakati.” Amesema Mduma
Mafunzo ya tathmini za ulemavu uliotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi ni endelevu, ambapo WFC mafunzo hayo kwa madaktari katika mwaka wa fedha 2015/16. Mpaka sasa, tayari jumla ya madaktari 1,301 kutoka wilaya mbalimbali hapa nchini wameshapatiwa mafunzo. Aidha, WCF imeshafanya mafunzo ya aina hiyo katika Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za juu Kusini na Kanda ya Pwani.
Mwaka 2015, serikali ilianzisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa lengo la kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanaoumia kazini au kupata magonjwa yatokanayo na kazi wanapata mafao bora ya fidia kwa ajili ya kuwawezesha kumudu maisha yao tofauti na utaratibu wa fidia uliokuwepo chini ya Sheria ya zamani ya Fidia kwa Wafanyakazi ya mwaka 1949.