……………………
Na Lucas Raphael,Tabora
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imetakiwa kuweka utaratibu wa kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mapokeo ya teknolojia zilizokwisha sambazwa na kupata mrejesho kutoka kwa wakulima na wadau mbalimbali unaoakisi malengo ili kuona tija iliyopo katika uhaulishaji teknolojia hiyo kwa wakulima nchini.
Agizo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani katika hotuba yake iliyosomwa kwa niamba yake na mkuu wa wilaya ya Tabora mjini Dkt Yahya Nawanda katika Siku ya Mkulima iliyoandaliwa kwa pamoja na Vituo vya TARI Tumbi na Kihinga, iliyofanyika katika Kituo Mahiri cha usambazaji teknolojia bora za kilimo cha Fatma Mwasa kilichopo Ipuli Mkoani Tabora.
Alisema kwamba TARI kupitia vituo vyake 17 vilivyopo nchini vimekuwa vikifanyatafiti mbalimbali za kuzalisha teknolojia za kilimo zenye manufaa makubwa kwa wakulima na wadau wa kilimo.
Hata hivyo aliwataka wakulima waitumie kupata elimu sahihi kuhusiana na kilimo cha mazao mbalimbali pamoja na kujionea kwa vitendo vipando vya mazao vilivyopo katika shamba la kituo.
“Pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na TARI katika utafiti wa kilimo hapa nchini, TARI mna jukumu la kusambaza teknolojia bora za kilimo zitakazojibu hoja na changamoto za wadau wetu hususan wakulima pamoja na kuweka vifaa vya kupimia udongo na afya ya mimea na kutoa majibu papo kwa papo ili kusaidia kilimo chetu kiwe na tija kubwa”, alisema Balozi Dkt. Batilda
Aidha mkuu huyo wa mkoa alikipongeza kituo cha TARI Tabora kwa kuona hitaji la wakulima na kuamua kuanzisha Kituo hiki mahiri cha usambazaji teknolojia cha Fatma Mwasa Mkoani Tabora, kituo ambacho kinasaidia wakulima kwa nyakati tofauti wanapohitaji kupata elimu na teknolojia bora za kilimo, badala ya kusubiri maonyesho ya Nane nane ambayo hufanyika mara moja kwa mwaka.
Akizungumzia swala la Maafisa ughani, Balozi Dkt. Batilda alisema hwawe ni daraja kubwa kati ya Watafiti wa teknolojia bora za kilimo na wakulima, kwani wana jukumu kubwa la kutoa elimu sahihi na kwa wakulima pamoja na kutoa ushauri kuhusiana na changamoto zinazowakabili wakulima.
Hata hivyo alisema kwamba kila Halmashauri hihakikishe wana maafisa ughani wa kutosha kwa ajili ya kuwasaidia wakulima, ila nao maafisaa ughani wanapaswa kwenda na wakati kwa kupata elimu kutoka TARI kuhusiana teknolojia bora za kilimo zilizofanyiwa utafiti, na waitumie elimu hiyo kuwanufaisha wakulima katika maeneo yao
“Maafisa ughani nashauri waje kupata elimu hapa TARI Tumbi Miongoni mwa teknolojia nilizojifunza ni pamoja na matumizi sahihi ya mbegu bora, kupanda kwa nafasi, matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu na njia mbadala za kurutubisha ardhi kwa kutumia miti na mimea jamii ya mikunde. Teknolojia nyingine ni mbinu bora za kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno na uongezaji thamani katika mazao,” alisema Balozi Dkt. Batilda
Kwa upende wake, Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Tumbi Tabora ,Dkt. Emmanuel Mrema alisema lengo kubwa la kuwa na kituo hicho mahiri ni kutoa mafunzo ya kilimo bora kwa wadau kama vile matumizi sahihi ya mbolea, viuatilifu na kilimo hifadhi kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kutoa ushauri unaozingatia utunzaji wa mazingira kwenye shughuli za kilimo ili kuokoa muda na nguvukazi kwa kuwa na namna bora ya kuandaa mashamba, upandaji, palizi, uvunaji na usindikaji ili kuongeza ubora na thamani wwa bidhaa za mazao.