Adeladius Makwega-DODOMA
Kabila la Wamaasai ni miongoni mwa makabila yanayopatikana katika mataifa ya Tanzania na Kenya. Tanzania wanapatikana katika maeneo ya Longido, Loliondo, Ngorongoro, Monduli, Kibaya na eneo la Nabereza. Nchini Kenya wakipatikana katika maeneo ya Londiani, Naivasha, Narok, Kajiado na Namanga.
Kwa hesabu za namba ikiaminika kuwa asilimia 10 ya mataifa haya mawili yanakaliwa na Wamasai. Eneo wanalopenda kuishi huwa ni tambalale, linalofaa kwa uchungaji, kwa Kimaasai linaitwa OLVURKEL likimaanisha eneo lenye majani ya kutosha kwa ajili ya mifugo.
Wamasai ni kabila linalofahamika kama NILO HAMITIKI wakiwa mabingwa wa wakupigana na kazi yao kubwa ni ufugaji wa mifugo.
“Kukiwa na dhana kuwa Wamaasai huwa hawaibi mifugo, bali wanakuja kuchukua mifugo yao pale wanapokuibia. Dhana ikiwa mifugo yote duniani ni ya Wamasai.”
Haya yanasema na J.Benne katika mojawapo ya maandishi yake ya utani kwa kabila hili.
Kwa Kimaasai kuna maneno mawili yanayomaanisha utani nayo ni ANGALAA huku ilikimanisha kumliza mtu. Lakini neno ENGIMALARE nalo likimaanisha kuwa huo ni utani. Neno ENGIMALARE likimaansha kumpa mtu zawadi na wakati huo huo hupatiwa jina. Hapo ndipo utani wa watu hao wawili unaanza. Kwa mila ya Kimaasai kila jambo huwa linachukuliwa kwa umakini.
Hata katika ngoma Morani wanaweza kucheza na hapo unaweza kuibuka ugomvi mkubwa usiotegemewa. Ndiyo maana hata neno ENGALAA linatajwa kama neno ya utani kama nilivyokwambia awali huku maana yake ni liza mtu.
Kwa mila za Kimaasai mgawanyo wa kazi huwa kulinga na rika za wahusika. Wavulana wakiwa na jukumu makubwa zaidi ya wasichana hasa la ulinzi wa jamii hiyo, kwani mara baada ya kutahiriwa huwa ni watu wazima na ukabidhiwa majukumu makubwa.
Kazi ya kupewa majaribio kama kwenda kuiba mifugo ya majirani zao au kwenda kumsaka Simba au Chui msituni na kumuua hutolewa.
Kabila hili huwa na mkubwa zaidi ya wote naye ni OLOIBONI.
Mathalaini kama vita vinatokea Oloiboni hufuatwa ili yeye aweze kusema kama vita hivyo watashinda na kuweza kutoa hirizi ya kuwalinda wakiwa vitani.
Hata mvua inapokosekana hufuatwa ili yeye atoe mwongozo wa kupata mvua, yeye hufanya maombi maalumu ya kuwaongoza kupata mvua.
Wamaasai wanapakana na makabila mengi yakiwamo Wakikuyu, Wakamba, Wambulu, Wanandi, Waarusha,Wameru, Wagogo, Wachaga na Wasonjo.
Utani huo wa ENGIMALARE na ENGALAA shabaha yake ni kuongeza urafiki baina yao. Pia utani huo unaaminika unasaidia kuondoa laana ambayo huleta KIFO kinachosababishwa na pepo mbaya (ILMENENGA) na matendo mabaya.
Je kipi kitaendelea ?