Arusha.Jumla ya kiasi cha shs 256.8 bilioni kinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa bandari ya Tanga kwa awamu ya pili wa ujenzi wa gati la kwanza na pili ambapo kwa Sasa umefikia asilimia 26 na unatarajiwa kukamilika kwake ni Oktoba ,16,2022.
Akizungumza na waandishi wa habari,Mhandisi Hamis Kipalo amesema mradi huo umefikia asilimia 26 lakini pamoja na matarajio hayo ya kukamilika kwa mradi huo Mkandarasi yupo nyuma ya muda hivyo inasadikika ataongezewa muda wa utekelezaji wa mradi huo.
“Mkandarasi yupo nyuma ya muda kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa Covid -19 ambapo nchi nyingi zilifungwa na baadhi ya vifaa huagizwa nje ya nchi,”amesema Mhandisi Kipalo.
Ameongeza kuwa, mradi huo una urefu wa mita 450 na upana mita 50 ambapo utekelezaji wale ulianza Septemba 5,2020 na utatekelezwa ndani ya miezi 22.
Amesema pamoja na mkandarasi huyo kusadikika kuongezewa muda kutokana na changamoto hizo pia atakabidhi kipande cha mradi chenye urefu wa mita 150 kati ya 450 ili kuweza kuanza kazi.
Mhandisi Kipalo ameongeza kuwa mradi huo utaleta manufaa kwa wananchi na wafanyabiashara katika kuongeza ufanisi wa bandari kutoka tani laki saba na nusu hadi tani milioni tatu ambapo uwezo wa bandari utaongezeka na kufanyika haraka tofauti na mwanzoni.
Amefafanua kuwa,kutokana na kuongezeka kwa ufanisi wa bandari hiyo pia kutasaidia kufanyika kwa biashara katika ukanda wa kaskazini na Afrika ya mashariki hali ambayo itaongeza wateja,”amesema.
Hata hivyo mradi huo unatekelezwa na kampuni ya CHEC kutoka China na kusimamiwa na Kampuni ya NIRAS kutoka Denmark ikishirikiana na kampuni ya kitanzania ya ANOVA.