Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Mkutano wa Bunge kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023 uliofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa, Bungeni jijini Dodoma, Machi 11, 2022. Kulia ni Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson na kushoto ni Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azan Zungu. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson katika Mkutano wa Bunge kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2022/2023 uliofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa, Bungeni jijini Dodoma, Machi 11, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya Wabunge wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua Mkutano wa Bunge kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2022/2023 uliofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa, Bungeni jijini Dodoma, Machi 11, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 kwenye ukumbi wa Msekwa, Bungeni jijini Dodoma, Machi 11, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa miradi pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa bajeti yake ili rasilimali zilizopo ziweze kuwa na tija inayoendana na thamani ya fedha za walipa kodi.
“vipaumbele muhimu vitaendelea kuzingatiwa ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya utoaji wa huduma kwa wananchi sambamba na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Machi 11, 2022) wakati akifungua Mkutano wa Bunge kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti wa Serikali kwa Mwaka 2022/2023 uliofanyika kwenye ukumbi wa Msekwa Bungeni jijini Dodoma
Mheshimiwa Majaliwa amesema ni azma ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuona ukomo wa bajeti hauathiri utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa sambamba na shughuli zilizopangwa kwa mwaka 2022/2023.
“Sote tunafahamu nchi yetu sasa iko katika uchumi wa kati ambayo ni ishara ya kuongezeka kwa uwezo wa Taifa kugharamia huduma muhimu kwa wananchi sambamba na kuongezeka kwa uwezo wa wananchi kumudu mahitaji yao.” Alisema.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa taarifa ya Utekelezaji wa Uhifadhi katika eneo la Ngorongoro ambapo amesema kuwa Serikali imeendelea kusimamia suala hilo kwa umakini mkubwa ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na wananchi na viongozi wa maeneo hayo ili kuhakikisha wanapata uelewa wa kutosha kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na wabunge.
“Tumefanya jitihada kubwa ya kuwaelimisha, kuwaeleza umuhimu wa uhifadhi na wao wamekuwa na ushirikiano mkubwa, Tumepata nafasi ya kukutana na viongozi wa viongozi wa kimila wa wamasai Malaigwanak zaidi ya 350. Viongozi hao wanawawakilisha wamasai wa nchi nzima na tumezungumza nao na wametuahidi kutupatia ushirikiano ili kupata suluhisho la kudumu katika maeneo yote yenye changamoto.”
Amesema hadi sasa Serikali imepokea orodha ya majina ya awali ya kaya 86 zenye watu 453 ambao wamekubali kuondoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari yao huku wengine wakiendelea kujiandikisha.
“Serikali imetenga eneo la hekari 400,000 lililoko katikati ya maeneo ya Wilaya za Handeni, Kilindi, Kiteto na Simanjiro na hekari 220,000 tayari zimepimwa viwanja 2,406 ambapo kati ya hivyo, viwanja 2,070 tumeandaa kwa ajili ya makazi na kila kimoja kina ukubwa wa ekari tatu. Tumeanza na nyumba101 zenye vyumba vitatu vya kulala kwa wale wanaotaka. Tuna viwanja 336 kwa ajili ya huduma kama shule za msingi na sekondari, zahanati na vituo vya afya. Ujenzi wa mifumo ya maji kazi inaendelea.”
Alisema na kuongeza kuwa, “Kila mwananchi atapewa eneo la heka tatu ili aweze kujenga boma na kuwa na eneo la ufugaji, eneo hili lina hali ya hewa nzuri na linaweza kulisha mifugo msimu wote wa masika na kiangazi.”
Waziri Mkuu amewataka wanasiasa walioko nje ya eneo la Ngorongoro waiache Serikali izungumze na wananchi walioko katika maeneo yale ili elimu na uhamasishaji wa wanaotaka kuhama kwa hiari wafanye wenyewe bila kushinikizwa na mtu yoyote na wale ambao wako tayari kuhama wasizuiliwe.
“Hakutakuwa na nguvu itakayotumia wala ukiukaji wa haki za binadamu, lakini ni matumaini yetu wenzetu walioko pale wataheshimu matazamio ya Watanzania ili kutunza uhifadhi na utalii ili mapato yanayopatikana na utalii katika eneo hilo yawanufaishe Watanzania wote. Tutaendelea kuwaelimisha ili waendelee kuondoka kwa hiari.”
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba, amesema hali ya uchumi imeendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha kuanzia Septemba 2020 hadi Januari 2021, ukuaji wa uchumi wa Taifa ulikuwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2020.
“Kuendelea kuimarika kwa hali ya uchumi jumla ni matokeo ya Serikali ya awamu ya Sita kuchukua jitihada mbalimbali ikiwemo kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, hususan utashi wa kisiasa wa kufanya mazungumzo na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Kasi kubwa ya miradi ya maendeleo na kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika miradi ya maendeleo na utekelezaji wa miradi na utekelezaji wa mpango wa kukabiliana na hali hasi ya Uviko 19.”
Aliongeza kuwa mradi wa ujenzi wa bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere umefikia asilimia 55 na shughuli za ujenzi zinaendelea, pamoja na ujenzi wa mradi wa treni ya mwendo kasi (SGR) pamoja na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka nchini Uganda.