Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Dadi Kolimba akizungumz a na Wajumbe wa Kikao cha Ujirani mwema kilichoandaliwa na NCAA na kufanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. John Mahu
Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Kamishna Msaidizi mwandamizi Johnson Laizer akizungumza na Wajumbe wa mkutano wa Ujirani mwema uliofanyika Wilayani Karatu
Washiriki balimbali wa mkutano huo wakiwa kikaoni.
Picha ya pamoja.
……………………………….
Na mwandishi wetu, NCAA
Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) leo tarehe 10 Machi, 2022 imefanya kikao na uongozi wa Wilaya ya Karatu kwa lengo la kujadili migongano ya wanyamapori na binadamu katika vijiji vinavyozunguka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Dadi Kolimba aliyeongoza kikao hicho ameipongeza Malaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa utaratibu wa kufanya vikao vya ujirani mwema ili kuweza kutoa mrejesho wa utekelezaji wa changamoto zinazosababishwa na migongano kati ya Wanyamapori na wananchi wa vijiji vinavyozunguka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
“Nimefurahi kuwa mnafanya vikao na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya pamoja na Madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi na kuwaeleza jitihada za Serikali kukabiliana na changamoto za wanyamapori wanaovamia maeneo ya Wananchi lakini pia wananchi kuvamia shoroba za Wanyama na kulima karibu na mipaka ya hifadhi”
Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Bw. Johnson Laizer ameeleza kuwa kikao hicho ni muendelezo wa kutoa mrejesho wa namna NCAA kwa kushirikiana wadau wa Uhifadhi inavyotatua changamoto za migongano ya binadamu na Wanyamapori.
Katika kikao hicho mada zilizowasilishwa ni pamoja na elimu ya kutatua migongano ya wanyamapori na binadamu, jitihada za NCAA kwenye utatuzi wa migongano baina ya wanyamapori na binadamu, sheria inayohusu kifuta machozi/jasho kwa wanyamapori hatari na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Bw. Karia Rajabu kupitia kikao hicho ameiomba serikali kupitia NCAA kuweka bajeti kwa kila mwaka wa fedha ili kuongeza jitihada za utoaji wa mafunzo kwa wananchi kuhusu mbinu mbalimbali za kukabiliana na Wanyama hatarisi.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mkurugenzi wa Halmashauri, kamati ya Ulinzi na usalama, Mbunge wa Karatu, baadhi ya Viongozi wa NCAA, Mkuu wa Hifadhi ya ziwa Manyara, waheshimiwa madiwani na baadhi ya menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.