Mkurugenzi Mtendaji wa Nipe Fagio, Ana Le Rocha akizungumza na waandishi wa habari wakati alipowasilisha utafiti wa uchafuzi wa mazingira taka ngumu katika mkutano uliofanyika ofizi za Nabaki Afrika Mwenge jijini Dar es Salaam leo.
………………………………………..
WAKATI Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikizidi kupambana katika kukabiliana na suala la kulinda mazingira hususan kuzuia matumizi ya plastiki, lakini imebainika kuwa kuna kampuni kubwa 10 ambazo ni vinara zinazoendelea kuzalisha bidhaa hizo.
Hayo yamebainishwa na Taasisi ya Nipe Fagio ambayo imekuwa ikifanya kazi za kusafisha maeneo ya fukwe na kutembelea maeneo ya jamii kuanzia mwaka 2018, 2019, 2020, na 2021, kwa ushirikiano na washiriki 32,151, Nipe Fagio ili kuangazia muundo wa taka nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi hiyo, baada ya kutembelea maeneo zaidi ya 350,000 na kuchambua vipande vya taka, matokeo yanaonyesha kuwa kwa wastani, asilimia 64 ya taka kwenye mifuko ya sampuli iliyokaguliwa ni taka za plastiki.
Mbali na hili katika kipindi cha mwaka 2021 taka za plastiki zilichangia asilimia 76 ya taka zote zilizokusanywa, asilimia 42 zikiwa ni taka zitokanazo na makampuni mbali mbali.
Akizindua matokeo ya utafiti wao kwa kipindi cha mwaka mwaka 2021, wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo,
Mkurugenzi Mtendaji wa Nipe Fagio, Ana Le Rocha, amesema kupitia utafiti wao ambao waliufanya kwa muda wa miaka minne umeweza kuonyesha kuwa wazalishaji wa ndani ndio wanaoongoza kwa uchafuzi wa mazingira ambapo asilimia 75 ya taka zote zilizokaguliwa huku bidhaa za nje zikichukua asilimia 25.
“Uchambuzi wetu umebaini kuwa kuna zaidi ya makampuni wachafuzi wa mazingira 10 wanaoongoza kwa uchafuzi wa plastiki nchini yanayotengeneza vinywaji laini na kuhifadhi kwenye chupa za platiki hivyo kuchangia pakubwa katika suala zima la uchafuzi wa mazingira.
Rocha alifafanua kuwa mwaka wa 2021, umekuwa mwaka muhimu zaidi wa kufanya mashirika yanayozalisha plastiki kuwajibika kwa mchango wao katika mabadiliko ya hali ya hewa wakati viongozi wa duniani na kwamba walikutana katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) kujadili jinsi ya kupunguza joto duniani. 1.5°C.
Mnamo mwaka 2022, tulipata azimio la “Kukomesha Uchafuzi Utokanao na Plastiki Kuelekea Azimio la kisheria la kimataifa” lililoidhinishwa katika mkutano wa UNEA 5.2 na kuchukuliwa kuwa ni makubaliano muhimu zaidi kuchukuliwa tangu makubaliano ya Paris.
Azimio hili linalenga mzunguko mzima wa maisha ya plastiki, kutoka uzalishaji hadi utupaji, na inatambua umuhimu wa Waokota Taka na wafanyakazi wasio rasmi kwa kurejesha taka.
“Kwa mujibu wa uchambuzi wa taka na chapa tulioufanya katika kipindi cha miaka 4 kati ya 2018 na 2021, tuligundua kuwa kuna kampuni mbili za Tanzania ambazo zimeongoza kwa kuwa wachafuzi wakubwa kutokana na kuzalisha chupa za plastiki nchini.
“Kuchambua takwimu tulizonazo mkononi, kwa hali ya kawaida haitoshi tu kutegemea juhudi za urejeshaji taka pekee ili kushughulikia uchafuzi wa mazingira na mgogoro wa hali ya hewa unaosababishwa na vifaa hivi vya plastiki vinavyotumika mara moja,“aliongeza.
“Tunahitaji sana hatua kali kuchukuliwa na kufuatwa ili kuepuka kuiangamiza nchi kwa taka za plastiki zinazotumiwa mara moja wakati tunapozalisha na huu ndio mfano halisi,“ alibainisha zaidi.
Alisema kuwa upande usio wa haki wa hali hii ya plastiki ni kwamba vijana wa nchi hii watarithi mazingira ambayo yanakabiliwa na hali mbaya ya hali ya hewa kutokana na uchafuzi wa plastiki, ingawa wamekuwa na mchango mdogo katika hali hiyo.
Rocha alipongeza juhudi za serikali katika kukabiliana na uchafuzi wa mazingira kutokana na bidhaa za plastiki lakini pia akahimiza kwamba juhudi zaidi zinahitajika ili kukomesha tatizo la matumizi hayo.
“Tunafahamu na tunathamini hatua ambazo serikali tayari imechukua kupunguza matumizi ya plastiki. Hasa kwa kupigwa marufuku kwa mifuko ya mboga ya plastiki na marufuku inayotarajiwa ya kanga laini za plastiki zinazofunika chupa za vinywaji vya plastiki na chupa,“aliongeza.
Amesema kwamba hata hivyo wanaamini jitihada zaidi zinaweza kufanyika ili kumaliza tatizo hilo.“Kama raia wa kimataifa, hatuwezi kuendelea kutegemea nishati ya mafuta, hasa yale ambayo yanabadilishwa kuwa bidhaa za plastiki kwa ajili ya matumizi ya moja kwa moja ambazo zinaenea katika jamii zetu,“ameongeza.
“Kwa sababu hii, tunazihimiza serikali zetu za kitaifa kutoa wito kwa watengenezaji/wazalishaji wa plastiki wa matumizi ya moja kwa moja kufichua kiwango kamili chanzo cha plastiki zao ili kuweza kupunguza hali hii na kusaidia kutekeleza kwa kiasi kikubwa malengo yatakayofikiwa katika siku za usoni, na kuunda upya mifumo ya utoaji wa bidhaa zao badala ya vifurushi vinavyoweza kutumika tena na visivyo na plastiki,“ alihimiza.