Mkuu wa Chuo Kikuu cha Jordan, Profesa Betram Mapunda, (kulia), akibadilishana hati ya makubaliano ya kuwa mlezi wa taasisi ya EMFERD na Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi ya EMFERD, Padre Joseph Torondo mjini Morogoro jana. Picha na Victor Makinda.
………………………
NA VICTOR MAKINDA: MOROGORO
Chuo Kikuu cha Jordan, (JUCO) cha mjini Morogoro, kimeingia makubaliano ya miaka mitano ya kuwa mlezi wa taasisi ya Kumbukumbu ya Erick inayojishughulika na kutoa elimu na marekebisho kwa watoto wenye ulemavu ( EMFERD).
Akizungumza wakati wa kutiliana saini makubaliano hayo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Betram Mapunda, alisema kuwa chuo cha Jordan kitashirikiana na taasisi hiyo katika nyanja za elimu, misaada ya kijamii na mafunzo kwa watendaji wa taasisi ya EMFERD.
Profesa Mapunda alisema kuwa chuo cha Jordani kina wataalamu wa kada nyingi ikiwemo kada ya sheria na saikolojia hivyo wataalamu hao watakuwa msaada mkubwa kwa taasisi hiyo.
“ Chuo Kikuu Jordan ni taasisi ya wasomi yenye dhima kubwa ya kuisaidia jamii kupambana na changamoto mbali mbali pamoja na ustawi wa jamii hiyo.” Alisema Mapunda.
Profesa Mapunda alisema kuwa chuo hicho kimekubali kuwa mlezi wa taasisi ya EMFERD baada ya kuridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na taasisi hiyo ya kutoa malezi, elimu na stadi mbali mbali za maisha kwa watoto wenye ulemavu, hivyo anaamini kuwa taasisi hiyo inahitaji mchango wa wana taaluma hao ili kuiwezesha kutoa huduma hiyo kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza baada ya kutiliana saini hati hiyo ya makubaliano Mwenyekiti wa Bodi ya usimamizi wa taasisi ya EMFERD, Padre Joseph Torondo, alisema kuwa taasisi yake inatarajia kuboresha huduma sambamba na kupanua huduma kwa watoto wenye ulemavu
Naye Muasisi wa taasisi ya EMFERD, Josephine Bakhita, alisema kuwa ustawi wa watoto wenye ulemavu ni jukumu la jamii nzima hivyo alitoa wito kwa jamii kushikiana kwa pamoja kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata mahitaji yao ya msingi ikiwa ni elimu, afya na malazi.
MWISHO