Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Afisa Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Dkt Shogo Mlozi Sedoyeka, amesema kuwa Chuo hicho kinaendelea kutoa mafunzo hayo ambayo yamefadhiliwa na MPANGO WA MAENDELEO KWA USTAWI WA TAIFA NA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19, kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na kwamba mafunzo hayo yanatolewa katika mikoa nane ya Tanzania Bara ikiwemo Lindi, Mtwara, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Mwanza, na Mara, ambapo Mpaka Sasa tayari yameshatolewa katika mikoa sita na kwamba mikoa ya Mwanza na Mara ndio yamezinduliwa rasmi na kukamilisha idadi ya mikoa yote nane ifikapo Machi 11, 2022.
Dkt.Sedoyeka amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wanarudisha shughuli za utalii katika hali yake ya awali na kufikia malengo ya taifa ya kufikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025, kwa sababu ya janga la UVIKO-19 liliathiri sana sekta ya utalii.
Amesema UVIKO-19 iliathiri kwa kiwango kikubwa Sekta hiyo na watalii kupungua kutoka milioni 1.5 mwaka 2019 hadi 620,000 ambapo serikali kupitia chuo hicho imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo ya kutoa mafunzo hayo.
Aidha amefafanua kuwa serikali ilitoa fedha hizo kwa ajili ya mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwajengea uwezo watoa huduma wa Sekta hiyo na kupata uelewa wa namna ya kufanya shughuli zao kwa kufuata miongizo na kuchukua tahadhari katika kukabiliana na janga la UVIKO-19.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum Kalli, amesema Sekta ya Utalii imechangia kuongeza fedha za kigeni kwa taifa kwa asilimia 25 na zaidi ya asilimia 17 katika Pato la taifa pia kuchangia ajira milioni 1.6.
Kalli amesema,janga la UVIKO-19 limeathiri sekta ya utalii duniani ambapo kwa hapa nchini imeshuka pia, kuyumba kwa biashara za utalii kwa sasa katika sekta ya utalii nchini imeanza kukamilika.
Amesema serikali katika kutambua umuhimu wa sekta hiyo imeamua kutafuta suluhu za changamoto ambapo kupitia chuo cha Taifa cha Utalii kimeanza mafunzo kwa wadau wa utalii.
“Sekta ya utalii ni muhimu katika kukuza pato la taifa,fursa kwenu kualika wawekezaji waweze kuwekeza mkoani Mwanza katika sekta ya utalii kwani tunajukumu la kukuza mji wa Mwanza kwa kutengeneza fukwe ndani ya ziwa Victoria,” amesema Kalli.
Mwisho
PICHA MBALIMBALI ZA MATUKIO KATIKA UFUNGUZI WA MAFUNZO HAYO