Waziri wa ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa akiwa katika ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kukagua mradi wa ujenzi wa daraja la mto wami.
………………………..
Na Victor Masangu,Pwani
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameuagiza kuongezwa kwa kasi ya ujenzi wa daraja jipya la Wami na barabara zake unganishi kukamilisha ujenzi mapema kabla ya muda wake uliopangwa kukamilika ili hadi kufikia tarehe 15 mwezi wa julai mwaka huu.
Profesa Mbarawa amesema hayo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo lililopo Chalinze mkoani Pwani ambapo hadi sasa daraja jipya la Wami limekamilika kwa asilimia 71.
Profesa Mbarawa alisema Wakandarasi wa ujenzi wa daraja hilo, Mkandarasi Mshauri, Meneja wa Wakala wa Barabara mkoa wa Pwani TANROADS na Wataalamu wake wahakikishe kasi ya ujenzi huo inaongezwa ili hadi tarehe hiyo 15 mwezi julai yeye mwenyewe atakuja kukagua tena maendeleo ya ujenzi huo sambamba na kupitisha kwa mara ya kwanza gari katika daraja hilo jipya hivyo kasi ya ujenzi iongezwe.
Alisema daraja hilo lilitakiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu lakini Profesa Makame ameagiza daraja hilo jipya likamilike hadi tarehe hiyo 15 mwezi julai mwaka huu hatua daraja hilo ilipofikia ni matengenezo madogo madogo.
Alisema ujenzi wa daraja hilo jipya ni miradi muhimu lina urefu wa mita 510, barabara za kuunganisha na upana wa magari mawili kupishana.
“Kaz inaenda vizuri na kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa na tuna harakisha ujenzi wa daraja hili ili kuhakikisha changamoto zilizokuwepo kwenye daraja la Wami la zamani zinakwisha”
Alisema daraja la zamani linaurefu wa mita 3.7 huku daraja jipya la Wami linajengwa lina urefu wa mita 11.8 ambalo ni kama mara tatu ya daraja la zamani hivyo ajali zilizokuwa zinatokea kule hazitatokea kwenye daraja jipya.
“Kwahiyo naomba sana Mkandarasi, Meneja wa Wakala wa Barabara mkoa Pwani TANROADS mkoa wa Pwani, mkandarasi mshauri, na wataalamu waliopata fursa ya kufanya kazi hii tulimalize ujenzi wa daraja hili mapema”
“Daraja hili lilitakiwa likamilike mwezi Novemba mwaka huu lakini mimi tarehe 15 julai mwaka huu nataka nipate kwenye daraja hili nipitishe gari kwa mara ya kwanza, gari langu kwa mara ya kwanza litapita kwenye daraja hili ” alisema Profesa Mbarawa.
“Na sina wasiwasi kwani hili linawezekana kwa mara ya kwanza siku hiyo gari langu kwa mara ya kwanza litapita kwenye daraja hili na baada ya hapo tutaweka mpango maalumu wa namna ya kutumia daraja hili”
Alisema nia ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inataka wananchi watumie miundombinu hii ya kisasa katika kuliletea maendeleo taifa letu.
Aidha alisema anafarijika sana na maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo jipya.
Akizungumzia maendeleo yaliyofanyika katika kipindi cha mwaka mmoja ya utawala wa awamu ya sita tangu ulipoingia madarakani Profesa Mbarawa alisema kuna mengi yaliyofanyika kwa kujivunia.
“Kuna kukamilika kwa ujenzi na kuanza kutumika kwa daraja la tanzanite lenye urefu wa kilomita 5.8 ambalo limepunguza msongamano wa magari “
Pia alizungumzia daraja la kigongo Busisi Profesa Mbarawa amesema daraja hilo linaongoza kwa ukubwa katika Afrika mashariki na kati litaandika historia kwani lina urefu wa kilomita 3 linatarajiwa kukamilika na hakuna mradi utakaosimama.
“Haya yote ni kwasababu Rais Samia Suluhu Hassan anatusimamia vema tunafanya kazi kubwa, anatoa fedha kwa wakati nyinyi mmeona hili daraja jipya la Wami lilitakiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu lakini kitakamilika mwezi julai mwaka huu ni hakuna mradi utakao simama”
“Kuna miradi mingine 24 sasa mingine imeshasainiwa Tanzania nzima tukiwa tunahakikisha nchi nzima inafunguliwa sambamba na kuifungua Nchi na nchi za jirani kupitia barabara ya Bagamoyo kupitia Lamu ambapo kesho kutwa tutakuwa Tanga kufungua ujenzi ambapo fedha yake nayo ipo, Wakandarasi nao wapo na sisi tuna nia ya kusimamia ilikuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati” alisema Profesa Mbarawa.
Akizungumzia viwanja vya ndege amesema hivi karibuni wamesaini mkataba wa upanuzi wa njia za kutua ndege katika uwanja wa ndege wa Dodoma Msalato.
“Na pia hivi karibuni tunatarajia kusaini mkataba wa ujenzi wa kupata mkandarasi wa jengo la kukaa abiria la uwanja huo”
Kwa upande wa uwanja wa ndege wa Mtwara amesema Kazi inaendelea vizuri ambapo imefikia asilimia 84, ukienda Musoma ujenzi wa kiwanja cha ndege unaendelea vizuri na ukienda Songea ujenzi unaendelea vizuri umefikia asilimia 95 hiyo yote ni kwaajili ya usimamizi mzuri wa Rais Samia.
Kuhusu vivuko Profesa Mbarawa alisema wamejipanga vizuri ujenzi unaendelea vizuri.
“Miradi mingi inaendelea na hakuna mradi utakaosimama kukamilika kwake maana tuna simamiwa vizuri na Rais Samia tutahakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati” alisema.
Awali Meneja wa Wakala wa Barabara mkoa Pwani TANROADS Eng. Baraka Mwambage akitoa taarifa ya ujenzi wa daraja jipya la Wami alisema mkataba wa ujenzi ulisainiwa juni 28 mwaka 2018 na kazi za ujenzi zilianza miezi minne baadaye.