Na Sixmund J. Begashe
Serikali imeipatia Makumbusho ya MajiMaji jumla ya Shilingi Milioni Sitini (60,000,000/) ili kutekeleza mradi wa uboreshaji wa Makumbusho ya Majimaji Songea ambao unatarijiwa kuongeza ufanisi zaidi katika kutoa huduma kwa wageni watakao itembelea Makumbusho hiyo pamoja na kazi ya uhifadhi.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Bi Joyce Mkinga kwenye uzinduzi wa mradio huo ulio enda sambamba na Tamasha la kumbukizi ya Mashujaa wa Vita ya Maji Maji na Utalii wa Utamaduni kwa mwaka 2022
Bi Mkinga licha ya kuishukuru serikali chini ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuishika mkono Makumbusho ya Taifa, amesema mradi huo ni sehemu ya miradi 15 inayotekelezwa na Taasisi hiyo chini ya ufadhili wa Miradi ya Kuinua Ustawi wa Nchi na Mapambano dhidi ya UVIKO -19
Akizindua mradi huo, Naibu Waziri wa Tamisemi Mhe Divid Silinde (MB) licha ya kuipongeza Makumbusho ya Taifa chini ya Mkurugenzi Mkuu, Dkt Noel Lwoga kwa kazi nzuri zinazofanyika ameitaka Taasisi hiyo kuhakikisha inatumia fedha za mradi huo kama ilivvyo kusudiwa na si vinginevyo
”Natambua Wizara inafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi yote inayotekelezwa na Makumbusho ya Taifa ili kuhakikisha kuwa lengo la Serikali linafikiwa. Kutokana na juhudi hizi sina shaka kwamba Miradi hii niliyoizundua leo itatekelezwa kwa weledi na ufanisi kwa kuzingatia taratibu zote za matumizi ya fedha za umma” Mhe Silinde
Awali Mratibu wa Mradi huo ambaye pia ni Muhifadhi wa Makumbusho ya Majimaji Songea, Bw Baltazari Nyamusya alieleza kuwa fedha hizo zitakwenda kuboresha kumbi za maonyesho, stoo kwa ajili ya uhifadhi wa mikusanyo, na ujenzi wa choo utakao saidia kuweka mazingira mazuri kwa wageni watakao itembelea Makumbusho hiyo.
Sanjari na Uzinduzi wa mradi huo, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe David Silinde (MB) alifunga rasmi Tamasha la Kumbukizi ya Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni ambalo ni sehemu ya kuadhimisha miaka 115 ya Mashujaa waliopigania utu wa watanzania kutoka kwa wakoloni.