Dkt Padri Xaver Komba akizungumza na watalii wandani, wazee wa mila, MaChifu kwenye ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria ya chanzo cha Vita vya Majimaji kwa Mkoa wa Ruvuma
Chifu Emmanuel Zulu, akizungumza na watalii wandani, wazee wa mila, MaChifu kwenye ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria ya chanzo cha Vita vya Majimaji kwa Mkoa wa Ruvuma
Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Bi Joyce Mkinga, kwenye ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria ya chanzo cha Vita vya Majimaji kwa Mkoa wa Ruvuma
Wananchi mbalimbali wakiwa kwenye ziara ya kutembelea maeneo ya kihistoria ya chanzo cha Vita vya Majimaji kwa Mkoa wa Ruvuma
Wasanii wa ngoma ya Mashujaa ya kabila la Wangoni wakipamba siku maalam ya kabila hilo, Maposeni, Peramiho.
………………………
Na Sixmund Begashe
Uhifadhi wa historia ya mashujaa wetu kwa njia ya kuweka alama ni muhimu sana kwa kuwa alama hizo zitasaidia kuvikumbusha vizazi vya sasa na vijavyo kuhusu mashujaa hao huku kukifanyika matamasha ya mara kwa mara kama sehemu ya kuhamasisha kuwaenzi kwa vitendo.
Hayo yamesemwa na Dkt Padri Xaver Komba alipozungumza na watalii wa ndani, wazee wa mila, machifu wa makabila ya Kusini na Malawi, waliotembelea maeneo ya kihistoria ilipoanzia Vita vya Majimaji kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma eneo la Maposeni kwa Chufu Mputa Gama.
Dkt Komba alisisitiza kwa kushauri kuwa, jambo hili lifanywe na makabila yute nchini, Zambia, Malawi na kote kwenye utajiri wa historia ya Mashujaa kwani licha ya uhifadhi tu wa urithi huo wa kihistoria maeneo hayo yataongeza idadi ya vivutio vya utalii.
“Tusisubiri wageni waje kutujengea minara ya watu wao waliomwaga damuda hapa kwetu, bali na sisi tuamke na kuongeza kasi ya kusimamisha minara kwenye maeneo ambayo tunaona ndipo wazee wetu damu yao ilimwagika kwaajili yetu, wao wakiona tumefanya hivyo na tunaendelea na utaratibu wetu, watakuja tu kutalii” Aliongeza Dkt Komba
Akielezea namna Vita vya Majimaji ilivyo anza, Chifu wa Wangoni Emmanuel Zulu, ameelaza kuwa ni kutokana na Padri ,Fransiscus, kuchoma nyumba ya kuabudia ya kabila la Wangoni ijulikanayo kama MAHOKA ili kuwalazimisha watu wa kabila hilo kuacha kufuata mila na desturi zao.
“Wenzetu wa Kilwa walisha anza mapambano na Mkoloni, sasa sisi tulipo chokozwa kwa kuchomewa nyumba yetu ya Ibada ambayo ilikuwa ni kama Rada yetu ya kutuonesha mema na mabaya, hakika mzee (Mputa Gama) alichukizwa sana, sasa alipopata dawa ya Kinjekitile hapo ndipo hari ya mapigani ikainuka” Chifu Zulu
Chifu Zulu ameongeza kuwa historia ya Mashujaa izidi kuimarisha upendo, mshikamano, hari ya kupenda kazi, uzalendo kwa nchi yetu na Afrika kwa ujumla ili vizazi vijavyo viweze kuikuta historia yetu si kwa kusoma tu bali hata kwa kupitia matendo yetu mema.
Akizungumzia maadhimisho hayo ya miaka 115 ya Vita vya Majimaji na urithi wa utamaduni hasa kwa upande wa siku ya Wangoni, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Bi Joyce Mkinga amesema, Taasisi yake itaendelea kushirikiana na wananchi wa Ruvuma katika kuhakikisha historia hii adhimu inaendelea kuhifadhiwa.
“ Taasisi ya Makumbusho ya Taifa inafanya kazi kwa karibu sana na wazee wa mila wa Mkoa huu hasa katika kuhakikisha sikuu hii ya Wangoni inafanikiwa kwa maana siku hii licha ya kuwa kivutio kikubwa cha utalii pia watu wanapata nafasi ya kujifunza historia kutoka eneo husika” Bi Mkinga
Sherehe ya Siku ya Wangoni, usherekewa kila mwaka tarehe 25 Februari kama sehemu ya Maadhimisho ya Kumbukizi ya Vita vya Majimaji na Utalii wa Umaduni ambayo ni sehemu ya kuadhimisha miaka 115 ya Mashujaa waliopigania utu wa watanzania kutoka kwa wakoloni.