……………………….
John Walter-Kiteto
Baraza la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, limepitisha rasimu ya bajeti ya 31,542,315,632.41 bil kwa kipindi cha mwaka 2022-2023.
Akisoma rasimu ya mpango huo, Afisa mipango wa halmashauri hiyo Beatrice Rumbeli, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto, John John Nchimbi, alitaja vyanzo vya mapato kwa mwaka 2022-2023.
Alisema fedha hizo Mishahara, PE 16,057,197,430.00 bil, Matumizi ya kawaida, OC 1,523,151,232.41 bil, Miradi ya maendeleo 11,100,971,000.00 bil na fedha za matumizi mengineyo (OC) Bil ni 2,860,995,970.00.
Akisoma mapendekezo ya mpango wa Bajeti kwa mwaka 2022-2023, Rumbeli alisema Halmashauri imepanga kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka 2,275,096,000.00 bil hadi 2,860,995,970.00 bil, kutenga asilimia 10% kwa ajili ya vijana wanawake na walemavu.
Kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili kuwezesha wakulima kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha na ziada kwa ajili ya kuuza na kujipatia kipato.
Kuwezesha mifugo bora itakayowezesha wafugaji kufuga kisasa kwa lengo la kujipatia kipato na kupata mazao bora yatokanayo na mifugo kama vile nyama maziwa na ngozi.
Kuendelea na upimaji wa mipaka ya vijiji na taasisi za Serikali, kupima na kutenga maeneo ya malisho ya mifugo na kilimo ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji inayoweza kujitokeza.
Akizungumzia rasimu ya Bajeti Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Abdallah Bundalah amesisitiza kuwa mpango huo uliopitishwa uzingatiwe kulingana na mahitaji ya wananchi ambayo ni muhimu.
“Naomba nisema hapa, mpango huu tuliopendekeza waheshimiwa madiwani humu sisi tumezingatia mahitaji ya wananchi tunaowawakilisha huko tulikotoka kwa hiyo isitokee mtu mmoja kwa matakwa yake akaamua kubadilisha kilichopendekezwa na waliowengi humu” alisema Mwenyekiti Bundallah
Nao baadhi ya madiwani akiwemo Kosei Lehinga Kata ya Loolera, Rehema Cheleleu Viti Maalumu walisema wananchi bado wana changamoto kubwa na ambayo ina hitaji dhamira ya dhati kwa kiongozi kutimiza wajibu wake kuwatumikia.
Walitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wananchi wa Kiteto kuwa ni pamoja na miundombinu ya barabara kuwa mibovu, huduma Elimu kutokidhi haja kwa wanafunzi kuwa na uhaba wa waalimu, madarasa vyoo na nyumba za waalimu